NA SILIVIA AMANDIUS, KAGERA
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, amesema asilimia 34 ya wakazi wa mkoa huo wanakabiliwa na tatizo la udumavu, huku asilimia 45 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wakiwa na changamoto ya upungufu wa damu.
Kanali Kido amesema hali hiyo inahitaji kuongezwa kwa juhudi za Serikali na wadau katika kuimarisha lishe, akisisitiza kuwa lishe bora ni muhimu katika kuongeza uwezo wa watu kufanya kazi na kuchangia maendeleo ya taifa. Amesema utapiamlo unaweza kuongeza kiwango cha umaskini, licha ya kuwa changamoto nyingi za lishe zinaweza kuzuilika iwapo hatua stahiki zitachukuliwa.
Amesema Serikali itaendelea kuongeza uelewa kwa jamii pamoja na kuwahimiza watumishi na wadau wanaohusika na masuala ya lishe kuongeza juhudi katika kupunguza changamoto hizo. Kauli hiyo ameitoa leo Septemba 30, 2026, wakati wa kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe Awamu ya Tatu ulioanza mwaka 2022.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera kimewakutanisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Makatibu Tawala pamoja na Maafisa Lishe kutoka halmashauri zote nane za Mkoa wa Kagera.

