Ujumbe wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ukiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Profesa Othman Chande, umemtembelea Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Yakubu, katika Ubalozi wa Tanzania jijini Paris. Ujumbe huo pia umemjumuisha Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Abdul Katunzi.

Ujumbe huo uko Paris kushiriki mkutano wa Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO). Wajumbe wamemweleza Balozi Yakubu kuwa kupitia mkutano huo wamekutana na wadau muhimu kwa TBS na kujifunza mbinu bora za kuratibu viwango vya bidhaa zinazozalishwa Tanzania na zinazoingizwa nchini.

Balozi Yakubu ameipongeza TBS kwa mafanikio hayo na kuhimiza wataalamu wa Tanzania katika sekta ya viwango kujiandaa kuwania nafasi za uongozi na uwakilishi ndani ya ISO na taasisi za viwango za kikanda barani Afrika.

Amesema ushiriki wa wataalamu wa Tanzania katika nafasi hizo utaiwezesha nchi kutoa mchango mkubwa zaidi katika mijadala na maamuzi kuhusu viwango vya kimataifa. Pia utasaidia kuimarisha ulinzi wa walaji, ubora wa bidhaa na uwezo wa wazalishaji wa Tanzania kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.