Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Wadau wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali pamoja na Wataalamu kutoka serikalini wamekutana kujadili namna bora ya kulinda haki za mtoto wa kike hususani katika kuhakikisha ndoa za utotoni zinamalizika. 

Hayo yamejadiliwa kwenye mkutano uliondaliwa na Chama Cha Wanasheria Wanawake Tanzania (TAWLA) ambapo mkakati ni kubaini jambo gani linalokwamisha sheria hiyo kufanyiwa marekebisho.Akizungumza kwenye mkutano huo Septemba 29,2026 Mkurugenzi wa TAWLA, Wakili Tike Mwambiple amesema sheria ya ndoa ina vipengele vingi ambavyo vinapaswa kufanyiwa marekebisho hasa kipengele cha ndoa za utotoni.

Amesema kwa maisha ya kawaida mtoto wa miaka 14 au 15 hawezi kuhimiri mikikimikiki ya ndoa na kueleza kuwa hata watu wazima walio na miaka zaidi ya 40 ndoa inakuwa ngumu kuiendesha.

Kwa upande wake Meneja wa programu kutokea Jukwaa la Haki za mtoto Tanzania Rogasian Massue amesema wanatamani mabadiliko ya umri sahihi wa ndoa yaweze kutokea.

Amesema Sheria karibia 6 zinazomhusu mtoto wa kike zinahitaji kufanyiwa mabadiliko ambapo wanatarajia serikali itazame suala hilo ambapo akieleza kuwa wadau na jamii kwa ujumla asilimia kubwa wameridhia mtoto wa kike apewe haki ya kuolewa akiwa na umri wa miaka 18.