Na Andrea Kadege, WAF–Dar es Salaam

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesema Tanzania na Global Fund zimeingia katika hatua ya mwisho ya kukamilisha ruzuku mpya ya afya ya GC8, itakayolenga kuimarisha mapambano dhidi ya HIV, Kifua Kikuu (TB), Malaria na mifumo ya afya nchini.

Ametoa kauli hiyo leo Septemba 28, 2026 Jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa GC8 Grant-Making Mission, Bw. Tayari amesema mkutano huo wa siku tano unalenga kutatua masuala ya kiufundi, kifedha na utekelezaji yaliyosalia kabla ya kukamilisha nyaraka za ruzuku hiyo.

“Katika siku tano zijazo, jukumu letu ni kutatua masuala yaliyobaki ya kiufundi, kifedha na utekelezaji katika ruzuku za UKIMWI, Kifua Kikuu, malaria na mifumo himilivu na endelevu ya afya,” amesema Bw. Tayari.

Amesema Jopo la Mapitio ya Kiufundi limependekeza ombi la Tanzania la GC8 liendelee katika hatua ya maandalizi ya ruzuku, huku likibainisha maeneo yanayohitaji uangalizi zaidi, ikiwemo huduma za UKIMWI, matibabu ya Kifua Kikuu na mpango wa uendelevu wenye gharama unaoonesha matumizi yenye tija ya rasilimali.

Aidha, amesema mkutano huo utajadili mapengo ya huduma na bidhaa za afya, ufanisi wa matumizi ya rasilimali, pamoja na namna ya kuimarisha mafunzo, kujenga uwezo na usimamizi wa huduma. 

“Mafanikio ya kuanza kwa ruzuku mpya tarehe 1 Januari 2027 yanategemea uwezo wetu wa kukamilisha kwa uwajibikaji majukumu ya sasa na kutatua kwa wakati mahitaji yote ya utekelezaji,” amesema.

Amesema kuwa serikali ya Tanzania Chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia utekelezaji wa GC7 hadi Desemba 2026, huku programu za UKIMWI, Kifua Kikuu na malaria zikitakiwa kushughulikia kwa wakati maoni yaliyotolewa katika tathmini ya utendaji ya mwaka 2025.

Mkutano huo wa siku tano unatarajiwa kukamilisha maamuzi, majukumu na muda wa utekelezaji wa hatua zilizobakia, pamoja na kuweka mwelekeo wa mwisho wa kukamilisha nyaraka za ruzuku ya GC8 kabla ya kuanza kutekelezwa Januari 1, 2027.