MASHIRIKA yasiyo ya Kiserikali (NGOs) mkoani Mara yametakiwa kubuni vyanzo vya ndani vya mapato vitakavyoyawezesha kuwa na uendelevu katika utoaji wa huduma kwa jamii, badala ya kutegemea wafadhili.
Wito huo umetolewa Septemba 29, 2026 na Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Taifa la NGOs Mkoa wa Mara, wakati akitoa salamu za Baraza hilo katika Jukwaa la Mwaka la mashirika hayo.
Jukwaa hilo limefanyika katika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara mjini Musoma, likihudhuriwa na viongozi wa mashirika mbalimbali pamoja na viongozi wa Serikali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mgeni rasmi katika jukwaa hilo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi.
Rhobi amesema mashirika mengi yanakabiliwa na changamoto za kifedha katika utekelezaji wa miradi, hivyo yana wajibu wa kubuni vyanzo vya ndani vya mapato ili yaweze kuendelea kutoa huduma kwa jamii.
Amesema hali hiyo inatokana pia na wafadhili wengi wa nje kusitisha au kupunguza misaada kwa mataifa yanayoendelea, jambo linalozitaka NGOs kuwa na mikakati ya kuhakikisha zinaendelea kujiendesha.
Aidha, ameyaomba mashirika hayo kushirikiana na kujenga ubia madhubuti na Serikali, taasisi za kifedha, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Kwa upande wake, Ofisa Mradi wa Familia Imara kutoka Shirika la Kivulini Women’s Rights Organization, Rayness Peter, amesema kupitia mradi huo wamefanikiwa kupokea jumla ya kesi 25.
Amesema nyingi ya kesi hizo zimeripotiwa na wanaume wanaokabiliwa na changamoto kutoka kwa wenza wao.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, ameyataka mashirika hayo kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo.

