*Kiwanda chazalisha hadi kilo 500 za dhahabu kwa siku
*Tanzania, Qatar kujenga ushirikiano katika uwekezaji na uongezaji thamani madini
*Wafanyabiashara wa Tanzania wahamasishwa kutumia fursa za soko la kimataifa
Doha, Qatar
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, ametembelea Kiwanda cha Kusafisha Dhahabu cha Falcon Gold and Precious Metals Refinery kilichopo jijini Doha, Qatar, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutathmini fursa za uwekezaji na uongezaji thamani madini kati ya Tanzania na Qatar.
Dkt. Kiruswa ametembelea kiwanda hicho akiwa ameambatana na wafanyabiashara wa madini ya vito kutoka Tanzania kwa ajili ya kushiriki na kujifunza mbinu mbalimbali katika Maonesho ya Kimataifa ya Vito na Saa ya Doha (Doha Jewellery & Watches Exhibition – DJWE) 2026, yaliyoanza Septemba 28 hadi Oktoba 3, 2026.
Kiwanda hicho kina uwezo wa kusafisha hadi kilo 500 za dhahabu kwa siku, huku kikipokea malighafi kutoka nchi mbalimbali duniani kwa ajili ya kusafisha na kuongeza thamani kabla ya kuingia katika masoko ya kimataifa.
Ziara hiyo imelenga pia kujifunza kuhusu teknolojia, mifumo ya uendeshaji na fursa zilizopo katika biashara ya kusafisha na kuongeza thamani madini, hatua inayoweza kutoa uzoefu muhimu katika juhudi za Tanzania kukuza shughuli za uongezaji thamani madini nchini.
Awali, Dkt. Kiruswa alitembelea Ofisi ya Balozi wa Tanzania nchini Qatar, Mhe. Habibu Mohamed, ambako alipokea taarifa kuhusu shughuli za madini nchini humo, pamoja na fursa zilizopo za kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Qatar katika uwekezaji na uendelezaji wa sekta ya madini.
Mkutano huo pia umejadili namna Tanzania na Qatar zinavyoweza kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini kuongeza uwekezaji, biashara na uongezaji thamani wa madini kwa manufaa ya kiuchumi ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Balozi, Mhe. Mohamed amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kutembelea Qatar, akieleza kuwa nchi hiyo inaendelea kuweka mipango ya kimkakati ya kushiriki zaidi katika sekta ya madini, hususan katika maeneo ya uchimbaji na uongezaji thamani madini.
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Falcon Gold and Precious Metals Refinery, Nada Rashid, amesema kiwanda hicho kiko tayari kushirikiana na nchi mbalimbali, ikiwemo nchi za Afrika Mashariki, kwa kupokea malighafi ya dhahabu kwa ajili ya kusafishwa na kuongezwa thamani.
Amesema ushirikiano huo unaweza kutoa fursa kwa nchi zinazozalisha dhahabu kutumia miundombinu ya kisasa ya usafishaji iliyopo Qatar, kuongeza thamani ya madini yao na hivyo kuchangia kukuza mapato na biashara katika sekta hiyo.
Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa Madini ya Vito Tanzania (TAMIDA), Osman Abdulsattar ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuona umuhimu wa kuwashirikisha wafanyabiashara hao kushiriki ziara hiyo ili kujifunza mbinu bora za uongezaji thamani na uendeshaji wa biashara ya madini ya vito kupia Maonesho ya Kimataifa.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Tanzania kutafuta fursa za masoko, uwekezaji, teknolojia na ushirikiano wa kimataifa katika sekta ya madini, sambamba na kuongeza thamani madini yanayozalishwa nchini.

