Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Dkt.Toba Nguvila akifungua kongamano hilo jijini Arusha leo
Happy Lazaro, Arusha.
Arusha .Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha,Dkt.Toba Nguvila amesema utekelezaji wa programu ya unywaji wa maziwa shuleni unapaswa kuleta matokeo yanayoonekana kwa watoto, ikiwemo kuongeza idadi ya shule zinazotekeleza programu hiyo na wanafunzi wanaopata maziwa nchini kila mwaka.
Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akifungua kongamano la wadau wa maziwa kuelekea siku ya unywaji maziwa shuleni 2026 ,kongamano lililoandaliwa na Bodi ya maziwa Tanzania likiwa na kauli.mbiu ya “Nyumbani,Shuleni Maziwa kwa lishe bora.”
Amesema programu hiyo inaweza kuwa daraja linalounganisha elimu ya wanafunzi na soko la maziwa, kuongeza kipato cha wafugaji, kukuza uzalishaji na kuimarisha tasnia ya maziwa, hivyo Serikali na wadau wanapaswa kuweka mifumo itakayohakikisha uwekezaji huo unaleta manufaa kwa jamii.
Dokta Nguvila amesema uwekezaji unaotajwa kufikia Sh500 bilioni kupitia ushirikiano wa Serikali na wadau unapaswa kuonyesha matokeo halisi, hususan kwa watoto mashuleni, akitaka idadi ya shule na wanafunzi wanaopata maziwa iongezeke kwa kila mwaka.
Amesema hatua nyingine ni kuhakikisha wanafunzi wanapata maziwa bora na salama, huku shule zikitakiwa kuangalia uwezekano wa kuanzisha miradi ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ili kuwa na chanzo cha maziwa, pamoja na kushirikisha wadau wanaosambaza bidhaa hiyo.
Dkt .Nguvila amesisitiza amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mfumo wa usambazaji wa maziwa kutoka kwa wazalishaji hadi shuleni, huku akitaka wazazi, wafugaji, wasindikaji, wafanyabiashara na shule kuunganishwa katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo. Amesema mpango huo haupaswi kuishia kwenye maadhimisho, bali uwe na mikakati endelevu ya mwaka mzima.
Kwa upande wake Mtaalamu wa lishe mradi wa mageuzi ya Tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi(C-SDTP) Dkt . Mackrina Mombo aliyemwakilisha Mratibu wa mradi amesema kuwa , maziwa ni chakula muhimu kwa watu wa makundi yote na yana mchango mkubwa katika afya, lishe na uchumi, hivyo uzalishaji na usambazaji wake unapaswa kuzingatia usalama kuanzia yanapozalishwa hadi yanapomfikia mlaji.
Amesema si kila maziwa au bidhaa ya maziwa inayopatikana sokoni ni salama kwa matumizi, hivyo maziwa yanapaswa kupitia mnyororo unaofaa wa ukusanyaji, usafirishaji, uhifadhi na usindikaji, huku wazalishaji na wafanyabiashara wakitakiwa kuzingatia viwango vya ubora na usalama.
Dkt.Mombo amewataka wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa za maziwa na kuhakikisha wanatumia bidhaa zinazokidhi viwango, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya ya jamii na kuongeza imani ya walaji kwa bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Mradi huu wa C-SDTP unatekelezwa na wizara ya mifugo na uvuvi “amesema Dkt.Mombo .
Kwa upande wake Msajili wa bodi ya maziwa Tanzania,Prof.George Msalya amesema ,maziwa yanapaswa kuwa na ubora na virutubisho muhimu kama protini na mafuta kwa kiwango kinachokubalika, ili kumsaidia mlaji kujenga na kuimarisha mwili na kupata manufaa yaliyokusudiwa kutokana na unywaji wa maziwa.
Amesema elimu kuhusu ubora wa maziwa inapaswa kuimarishwa ili wananchi wajue wanachotumia, badala ya kuangalia mwonekano pekee wa bidhaa, huku wazalishaji wakitakiwa kuhakikisha maziwa yanakuwa salama na yenye viwango vinavyostahili.
Msalya amesema unywaji wa maziwa shuleni ni uwekezaji katika lishe, afya, ukuaji na ustawi wa watoto, hivyo programu hiyo inapaswa kupewa msukumo zaidi ili kuongeza idadi ya shule na wanafunzi wanaonufaika.
Amesema kaulimbiu ya mwaka huu “Nyumbani, Shuleni, Maziwa kwa Lishe Bora” inalenga kuhamasisha familia na shule kuhakikisha watoto wanapata maziwa, huku wazazi wakitakiwa kuwa mfano kwa watoto kwa kutumia maziwa na kuhakikisha yanapatikana pia nyumbani.
Ameongeza kuwa kuimarisha unywaji wa maziwa kutahitaji ushirikiano wa Serikali, wazazi, shule, wafugaji, wazalishaji na wadau wengine, kwa kuwa hatua hiyo inaweza kusaidia kujenga kizazi chenye afya bora na wakati huo huo kuimarisha soko la maziwa na kuongeza kipato cha wafugaji.
Msajili wa bodi ya maziwa Tanzania,Prof.George Msalya akizungumza kwenye kongamano hilo jijini Arusha leo

Mtaalamu wa lishe mradi wa mageuzi ya Tasnia ya maziwa na mabadiliko ya tabianchi(C-SDTP) Dkt . Mackrina Mombo akizungumza kwenye kongamano hilo

