Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma Marco Chilya akizunguza na madereva wa mabasi na wadau wengine wa usafirishaji katika Kituo Kikuu cha Shule ya Tanga Manispaa ya Songea. 

Dereva wa Mabasi ya Kampuni ya Super Feo aliyefahamika Kwa jina la Nyoni,akizungumza katika Kituo cha Mabasi Shule ya Tanga Manispaa ya Songea.
……………..,
Na Mwandishi Wetu, Songea
Madereva wa mabasi Mkoani Ruvuma wametakiwa kuendelea na huduma ya usafirishaji wa abiria kama kawaida, huku Jeshi la Polisi likiwahakikishia ulinzi na usalama katika maeneo yao ya kazi, kufuatia taarifa za baadhi yao kusitisha huduma hiyo kutokana na changamoto mbalimbali.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Marco G. Chilya, wakati alipokutana na madereva, abiria, wananchi na wadau wanaofanya usafirishaji katika stendi ya mabasi iliyopo Kata ya Shule ya Tanga, Manispaa ya Songea, Septemba 29, 2026.
Katika mazungumzo hayo, Kamanda Chilya amesikiliza changamoto zinazowakabili wadau hao na kueleza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Idara husika linaendelea kuchukua hatua za kuhakikisha mazingira ya usafirishaji yanakuwa salama na ya amani, ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo muhimu bila usumbufu.
Aidha, amewataka madereva kutokuwa na hofu na kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa kufuata sheria na taratibu, huku akisisitiza kuwa ushirikiano kati ya Polisi, madereva, abiria na wadau wengine ni muhimu katika kulinda usalama na kuhakikisha huduma za usafiri zinaendelea bila vikwazo.
Hatua hiyo imekuja kufuatia taarifa za baadhi ya madereva wa mabasi ya abiria kusitisha huduma ya usafirishaji kutokana na sababu mbalimbali, hali inayoweza kuathiri wananchi wanaotegemea usafiri huo katika shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo baada ya mazungumzo hayo, madereva waliendelea na safari zao kama kawaida kuelekea mikoa mbalimbali, hatua iliyowezesha huduma ya usafirishaji wa abiria kuendelea huku wananchi wakiendelea na shughuli zao bila usumbufu wa usafiri.
