Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Zanzibar iko tayari kuimarisha ushirikiano na Shirikisho la Urusi pamoja na sekta binafsi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo nishati, bandari na usafirishaji, utalii, elimu na utafiti, afya pamoja na Uchumi wa Buluu.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 28 Septemba 2026, alipokutana na ujumbe kutoka Shirikisho la Urusi ulioongozwa na Bw. Denis Agafonov, Mkuu wa Kurugenzi ya Wataalamu katika Ofisi ya Rais wa Shirikisho la Urusi pamoja na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar ina fursa kubwa ya kuimarisha ushirikiano na Urusi katika sekta ya nishati, hususan katika uzalishaji na upatikanaji wa umeme, matumizi ya vyanzo mbadala vya nishati pamoja na teknolojia ya nishati ya nyuklia. 

Amesema tafiti za awali za kisayansi zinaonesha uwezekano wa kuwepo kwa rasilimali za mafuta na gesi asilia Zanzibar, hususan katika maeneo ya baharini, hivyo Serikali iko tayari kushirikiana na kampuni za Urusi zenye utaalamu na teknolojia katika shughuli za utafutaji, uchunguzi na uendelezaji wa rasilimali hizo. 

Akizungumzia bandari na usafirishaji, Rais Dkt. Mwinyi amesema nafasi ya kimkakati ya Zanzibar inatoa fursa kubwa ya kuimarisha shughuli za biashara na usafirishaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huku akieleza kuwa ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani unaendelea na kwamba Zanzibar iko tayari kushirikiana na Urusi katika maeneo ya ujenzi, teknolojia na utaalamu wa uendeshaji wa bandari ili kuongeza uwezo Zanzibar kuwa lango muhimu la biashara katika ukanda huo.

Katika sekta ya utalii, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inalenga kuongeza idadi ya watalii kutoka Urusi, hususan kutokana na kuimarika kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Zanzibar na Moscow, sambamba na kuvutia uwekezaji zaidi katika miradi ya utalii.

Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji kutoka Urusi kwenye miradi ya kuongeza thamani ya sekta ya utalii, kukuza biashara na kupanua fursa za ajira kwa wananchi.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inalenga kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu na Urusi kwa kuongeza fursa za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Tanzania, kuendeleza tafiti za pamoja pamoja na kuanzisha vituo vya mafunzo ya ufundi stadi na utafiti.

Amesema ushirikiano huo unaweza kujikita pia katika sayansi na teknolojia za bahari, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono utekelezaji wa sera na mipango ya Uchumi wa Buluu Zanzibar.

Dkt. Mwinyi amesema Serikali pia iko tayari kushirikiana na Urusi katika kuimarisha sekta ya uvuvi kupitia teknolojia, utaalamu na uwekezaji utakaosaidia kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya baharini.

Katika sekta ya afya, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inalenga kuongeza matumizi ya teknolojia ya tiba kwa njia ya mtandao, ili kuwaunganisha wagonjwa waliopo katika vituo vya afya na wataalamu waliopo katika vituo vya afya na hospitali za rufaa.

Rais Dkt. Mwinyi ameushukuru ujumbe huo kwa kutembelea Zanzibar na kuonesha dhamira ya kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Shirikisho la Urusi, huku akisisitiza umuhimu wa kugeuza maeneo yaliyojadiliwa kuwa miradi yenye matokeo yanayoonekana.

Naye, Bw. Denis Agafonov amesema Urusi ina uzoefu na utaalamu mkubwa katika sekta mbalimbali, hususan nishati, na iko tayari kuendelea kujadiliana na Zanzibar kuhusu maeneo yenye fursa za ushirikiano na uwekezaji.