Mwalimu mkuu wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Arusha Alliance iliyopo mjini hapa ,Elimboto Raphael akizungumza na waandishi wa habari katika mahafali hayo 

Na Happy Lazaro, Arusha.

WAZAZI wametakiwa kuendelea kuwafutilia na kuwaongoza watoto wao wanaohitimu darasa la saba kwani bado wana umri mdogo na wanahitaji malezi na usimamizi wa karibu ili waweze kufikia ndoto zao.

Hayo yamesemwa jijini Arusha na Mwalimu mkuu wa shule ya mchepuo wa kiingereza ya Arusha Alliance iliyopo mjini hapa ,Elimboto Raphael wakati akizungumza katika mahafali ya 17 ya wanafunzi wa darasa la saba ambapo jumla ya wanafunzi 114 wamehitimu.

Amesema shule hiyo inafurahia kushirikiana na wazazi pamoja na wadau mbalimbali waliohudhuria mahafali hayo na kutoa mchango katika safari ya elimu ya watoto hao.

Elimboto ameongeza kuwa , ndoto za wanafunzi hao zinaweza kutimia iwapo shule na wazazi wataendelea kushirikiana katika kuwalea, kuwafuatilia na kuwaombea, kwa kuwa watoto hao wenye umri wa takribani miaka 12 na 13 bado wanahitaji mwongozo wa karibu kutoka kwa watu wazima.

“Nawasihi wazazi kuwaweka watoto karibu na Mungu, kwani elimu ya kitaaluma inapaswa kwenda sambamba na malezi ya kiroho na maadili ili kuwajenga watoto wenye hofu ya Mungu, utu na tabia njema.”amesema Elimboto.

Amesema dunia ya sasa inahitaji wasomi wenye maadili kwa sababu elimu pekee bila misingi ya uadilifu inaweza kutumiwa vibaya, akitoa mfano wa baadhi ya wataalamu wakiwemo wahandisi na madaktari ambao wanaweza kutumia taaluma zao kinyume na matarajio ya jamii.

“shule yetu hailengi kuwafundisha wanafunzi kwa ajili ya kufaulu mitihani pekee, bali inazingatia pia kile ambacho mtoto anatoka nacho baada ya kumaliza masomo, ikiwemo uwezo wa kujitegemea, kujisimamia na kutumia elimu yake kwa manufaa yake na jamii.”amesema Elimboto.

Amesema pamoja na shule hiyo kufanya vizuri kitaaluma na kupata mafanikio katika madaraja ya ufaulu, jambo kubwa zaidi kwao ni kuhakikisha kila mwanafunzi anayehitimu anakuwa na uwezo wa kukabiliana na maisha na kuwa mtu anayehitajika katika jamii.

Elimboto pia amewataka wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri wa shule hiyo wanapoendelea na hatua nyingine za elimu, kwa kuzingatia mafunzo ya kitaaluma, malezi na maadili waliyopata shuleni.

Amesema ushirikiano kati ya wazazi na shule ni msingi muhimu katika kuhakikisha watoto wanakuwa na mwelekeo sahihi,huku akiwataka wazazi kutowaacha watoto baada ya kuhitimu Darasa la Saba, bali kuendelea kuwashauri, kuwaombea na kuwapa mazingira yatakayowawezesha kufikia malengo yao.

Elimboto amesisitiza kuwa mafanikio ya mtoto hayaishii kwenye cheti cha ufaulu, bali yanapimwa pia kwa uwezo wake wa kutumia elimu, maarifa na maadili aliyoyapata katika kujenga maisha yake na kuchangia maendeleo ya jamii.

Aidha amewataka wahitimu kuendelea kuwa na nidhamu, bidii na hofu ya Mungu huku wakitambua kuwa kuhitimu Darasa la Saba ni mwanzo wa hatua nyingine ya safari yao ya elimu na maisha.

Kwa upande wake mgenirasmi katika mahafali hayo,Mwalimu Mishita Ezra aliyemwakilisha Mkurugenzi wa shule ya sekondari ya Arusha Science ,Prof Nuhu Hatibu amewataka wanafunzi hao kujiendeleza zaidi kwani kuhitimu darasa la saba sio mwisho wa maisha bali wanapaswa wazidi kujiendeleza kwa ajili ya kufikia ndoto zao .

Mishita pia amewataka wazazi kuendelea kukuza vipaji vya watoto wao kwa kuwaunga mkono katika.jitihada zao mbalimbali badala ya kuwakatisha tamaa jambo ambalo linawavunja moyo watoto wengi.