Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
WANANCHI wa Mtaa wa Njeteni, Kata ya Kwembe, Dar es Salaam, wamepewa matumaini ya kupata shule ya msingi ya Serikali baada ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Mbunge wa Kibamba, Anjela Kairuki, kusema ujenzi wa miundombinu ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele vinavyopaswa kupewa kipaumbele katika maeneo yenye mahitaji.
Akizungumza katika uzinduzi wa Siku ya Njeteni (Njeteni Day), Kairuki alisema Serikali imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa shule katika maeneo yenye uhitaji, hivyo wananchi wa Njeteni wanapaswa kuhakikisha taratibu muhimu, ikiwemo upatikanaji na uthibitishaji wa eneo, zinakamilishwa ili eneo hilo liweze kunufaika na mpango huo.
Alisema ujenzi wa shule hiyo utasaidia kupunguza changamoto zinazowakabili wananchi katika kuwapeleka watoto wao kupata elimu, hasa kutokana na ongezeko la wakazi na mahitaji ya huduma za kijamii katika eneo hilo.
Kairuki alisema pamoja na shule, Serikali itaendelea kuangalia mahitaji mengine ya miundombinu katika eneo hilo, ikiwemo barabara zinazounganisha wananchi na huduma muhimu, huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Sambamba na hayo, Kairuki pia, alisema Serikali itafuatilia pia changamoto ya barabara za njeteni, ikiwemo zinazounganisha eneo hilo na vituo vya huduma za afya, ili kurahisisha usafirishaji wa wagonjwa, dawa na huduma nyingine muhimu kwa wananchi.
Akizungumza kwa niaba wananchi wa Mtaa wa Njeteni,Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa huo Frank Muhina aliwasilisha changamoto ya ukosefu wa ofisi ya Serikali ya Mtaa, akisema kwa sasa shughuli za kiutawala zinafanyika katika chumba kimoja kilichopangishwa, hali wanayoeleza kuwa haiendani na mahitaji ya eneo hilo.
Akizungumzia ombi hilo, Kairuki alisema yuko tayari kusaidia kutafuta fedha za kuanza ujenzi wa ofisi hiyo, ikiwemo kiasi cha hadi Sh milioni 10, endapo eneo litapatikana na nyaraka zake zitakuwa zimekamilika na kuthibitishwa na mamlaka husika.
Aidha, wananchi waliomba Serikali kusaidia kujenga kituo kipya cha huduma ya kujifungulia, wakisema jengo lililopo lilijengwa takribani miaka 17 iliyopita kwa msaada wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), lakini halijawahi kutumika kutokana na kutokidhi viwango vinavyohitajika.
Walisema hali hiyo imewalazimu wanawake wajawazito kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma za kujifungulia, huku jengo la zamani likielezwa kuwa limechakaa na kuwa hatarishi kwa matumizi ya wananchi.
Wananchi pia waliwasilisha changamoto ya mifereji ya maji kuziba na kusababisha maji kutuama katika maeneo ya makazi, huku wakitaka hatua zichukuliwe kuboresha mifumo ya maji ya mvua na kuzuia athari kwa mazingira.
Sambamba na hayo Mwenyekiti wa Mtaa wa Njeteni Mhina aliwasisitiza wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi katika kuibua na kufuatilia changamoto zao, akisema utekelezaji wa miradi ya shule, ofisi ya mtaa, barabara na huduma za afya utahitaji ushirikiano wa wananchi na Serikali ili kuboresha maisha ya wakazi wa eneo hilo.

