Arusha. Serikali imewapa wiki mbili Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Waziri wa Fedha, Waziri wa Kilimo na Msajili wa Hazina kuandaa mpango wa kuanza kuwawezesha vijana 10,000 kwa mwaka kutoka fani mbalimbali kwa lengo la kujenga rasilimali watu yenye utaalamu na ujuzi unaohitajika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, alisema Tanzania haiwezi kufikia Dira 2050 bila kuwekeza katika rasilimali watu ili vijana wapate utaalamu na ujuzi unaohitajika katika ujenzi wa Uchumi. 

Akifungua Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi na Mashirika ya Umma (C-CEOs Forum 2026) unaofanyika Arusha kuanzia Septemba 28 hadi 30, Mhe. Ndejembi aliwaagiza viongozi hao kuja na mpango huo ndani ya wiki mbili, akisisitiza kuwa uwekezaji katika watu unapaswa kuwa sehemu ya utekelezaji wa Dira 2050.

“Tusipime mashirika ya umma kwa kiwango cha gawio wanachotoa pekee, bali kwa namna yanavyoongeza tija kwa vijana ambao ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa letu,” alisema wakati wa mkutano huo, unaoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (OTR) na kudhaminiwa na Benki ya Biashara Tanzania (TCB).

Alisema mpango huo unapaswa kuwahusisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ya utaalamu na kuwajengea uwezo ili waweze kushiriki katika kutekeleza malengo ya Taifa.

Mhe. Ndejembi alisema uwekezaji katika rasilimali watu ni msingi wa kuongeza tija, ubunifu na uwezo wa taasisi za umma kukabiliana na mahitaji ya uchumi unaobadilika.

Alisema matumizi ya teknolojia mpya, ikiwamo akili bandia na mifumo ya kidijitali, yanahitaji watu wenye ujuzi wa kuzitumia kuongeza ufanisi na ubora wa huduma.

Maagizo hayo yalikuwa sehemu ya mwelekeo mpana wa Serikali kwa taasisi na mashirika ya umma katika utekelezaji wa Dira 2050, yakizitaka kuongeza thamani ya mali na uwekezaji wa Serikali, kuimarisha ushindani na tija, kupunguza utegemezi, kuwekeza katika teknolojia na ubunifu, na kuhakikisha utendaji wao unazalisha matokeo yanayoonekana kwa wananchi.

Mhe. Ndejembi alisema taasisi hizo hazipaswi kuishia kulinda mali za Serikali, bali kuzitumia kuongeza thamani na kuleta manufaa zaidi kwa Taifa.

“Msije kuwa walinzi wa mali pekee; kuweni waongezaji thamani wa mali mlizokabidhiwa,” alisema, huku akiongeza kuwa taasisi za umma zinapaswa kuwa injini za mabadiliko ya uchumi badala ya kubaki katika utekelezaji wa majukumu ya kiutawala pekee.

Katika kuimarisha ushindani na tija, alitaka taasisi kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa huduma, kutumia rasilimali kwa ufanisi na kujenga uwezo wa kukabiliana na mazingira ya ushindani yanayobadilika.

Mhe. Makamu wa Rais pia alitaka kila taasisi ya umma kuja na mpango wa kukabiliana na athari za El Niño, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto hiyo.

Kwa watendaji wakuu, alisema uongozi unapaswa kupimwa kwa uimara na matokeo ya taasisi wanayoiacha nyuma, akisisitiza umuhimu wa kuandaa viongozi wa baadaye, kukuza vipaji na kujenga rasilimali watu yenye uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya uchumi wa siku zijazo.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, alisema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji sekta ya umma na sekta binafsi kufanya kazi kwa karibu kutokana na nafasi ya kila upande katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa.

“Utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji sekta ya umma na sekta binafsi kufanya kazi kwa karibu, kutokana na nafasi ya kila upande katika kufikia malengo ya maendeleo ya Taifa,” alisema Prof. Mkumbo.

Alisema Dira 2050 inalenga sekta ya umma kuchangia asilimia 30 ya uchumi, huku sekta binafsi ikitarajiwa kuchangia asilimia 70, hivyo mazingira ya biashara na uwekezaji yanapaswa kuwezesha sekta binafsi kukua.

“Ili sekta binafsi ifanye vizuri ni lazima taasisi za umma zitengeneze mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji,” alisema Prof. Mkumbo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Mhe. Masanja Kadogosa, alisema kamati yake inaridhishwa na kasi ya mageuzi yaliyofanyika na yanayoendelea katika taasisi za umma, lakini akasisitiza kuwa bado kuna safari ndefu ya kuboresha utendaji.

Mhe. Kadogosa alisema taasisi hizo zinapaswa kuendelea kuboresha shughuli zao za uzalishaji na kutengeneza mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki zaidi katika shughuli za kiuchumi.

“Tunapaswa kuendelea kuboresha shughuli zetu za uzalishaji na kutengeneza mazingira rafiki kwa sekta binafsi, lakini lazima muainishe mipango yenu na Dira 2050,” alisema Kadogosa, ambaye pia ni Waziri Mteule wa Ujenzi.

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, alisema mabadiliko hayo yanapaswa kwenda sambamba na namna mpya ya kupima utendaji wa taasisi na mashirika ya umma.

Alisema utendaji haupaswi kupimwa kwa gawio pekee, bali pia kwa tija, ubora wa huduma, matumizi yenye ufanisi ya rasilimali, uimara wa kifedha, ubunifu, matumizi ya teknolojia, uwezo wa kushindana na mchango mpana wa taasisi katika uchumi.

Bw. Mchechu alisema ongezeko la thamani ya uwekezaji wa Serikali na mapato yanayotokana na uwekezaji huo linaongeza wajibu kwa taasisi za umma kuhakikisha rasilimali hizo zinasimamiwa kwa ufanisi na kuendelea kuzalisha thamani.

Thamani ya uwekezaji wa Serikali katika taasisi na kampuni ambazo ina hisa chache imeongezeka kutoka Sh67.95 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh92.28 trilioni mwaka 2024/25, wakati mapato yasiyo ya kodi yaliyotokana na uwekezaji wa Serikali yameongezeka kutoka Sh637.7 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26.

Bw. Mchechu alisema mwelekeo huo unaifanya C-CEOs Forum kuwa jukwaa muhimu la kujadili namna taasisi za umma zinavyoweza kuongeza mchango wao katika uchumi na kuoanisha mipango yao na malengo ya Dira 2050.

Mkutano huo ni wa nne tangu kuanzishwa kwake mwaka 2023 na unawakutanisha zaidi ya washiriki 700 kutoka taasisi na mashirika ya umma, sekta binafsi, taasisi za fedha, wawekezaji, washirika wa maendeleo, wataalamu na wasomi.

C-CEOs Forum 2026 ina kaulimbiu, “Taasisi na Mashirika ya Umma yenye Ufanisi wa Juu kwa Uchumi Shindani, Jumuishi na Imara Katika Kutekeleza Dira 2050,” na inalenga kujadili uongozi, utawala bora, ubunifu, rasilimali watu, ushindani na namna ya kuongeza thamani ya kiuchumi na kijamii kupitia taasisi za umma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa (TCB), Adam Mihayo, alisema benki hiyo iko tayari kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutekeleza Dira 2050, akieleza kuwa TCB imeendelea kuelekeza mikakati yake katika kuunga mkono sekta za uzalishaji zinazoendana na malengo ya Dira hiyo.

Alisema TCB imekuwa ikifanya hivyo sambamba na mageuzi na ajenda ya kujenga uchumi inayosimamiwa na Serikali, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta binafsi katika kufanikisha malengo ya maendeleo ya muda mrefu.