Dodoma:
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imepiga marufuku matangazo yote yanayohamasisha matumizi ya dawa za kupunguza au kuacha unywaji wa pombe.
Dawa zilizotajwa kupigwa marufuku kutangazwa ni Naltrexone, Acamprosate na Disulfiram.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa leo Septemba 27, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dkt. Adam Fimbo, mamlaka imebaini baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vimekuwa vikirusha matangazo ya dawa hizo ambazo kisheria ni dawa zinazotolewa kwa cheti cha daktari pekee (Prescription-Only Medicines – POM).
Hali hiyo ni kinyume na Kanuni ya Makundi ya Dawa za Mwaka 2026 (Tangazo la Serikali Na. 150).
TMDA imesema matumizi ya dawa hizo bila ushauri wa mtaalamu wa afya yanaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo kifo, hasa zinapotumiwa pamoja na pombe au dawa nyingine.
“Kifungu cha 52 cha Sheria ya Dawa na Vifaa Tiba, Sura ya 219, kinakataza kutangaza kwa umma dawa yoyote inayotolewa kwa cheti cha daktari. Dawa hizo zinaruhusiwa kutangazwa kwa wataalamu wa afya pekee kupitia majarida ya kitaalamu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.
Kutokana na hali hiyo, TMDA imewaelekeza wafanyabiashara, watoa huduma za afya, wamiliki wa vyombo vya habari na waendesha mitandao ya kijamii kuacha mara moja kuandaa, kurusha na kuchapisha matangazo hayo.
Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa wanapobaini watu, vituo au vyombo vinavyotangaza dawa hizo kupitia ofisi za TMDA zilizopo maeneo mbalimbali nchini.
