Na Silivia Amandius
Kagera.
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera umetaja maeneo hatarishi yanayoweza kuathiriwa na mvua kubwa na mafuriko yanayotarajiwa katika kipindi cha mvua za El Niño, huku ukitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kuepuka maeneo yaliyo katika hatari.
Akizungumza mwishoni mwa wiki hii ofisini kwake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kagera, Mhandisi Christian Mbise, amesema maandalizi mbalimbali yamefanyika kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua hizo, ikiwemo kuweka mikakati ya kuimarisha miundombinu ya barabara na kuhakikisha maeneo hatarishi yanakuwa salama kwa watumiaji wa barabara.
Mhandisi Mbise amesema TANROADS imeendelea kufanya matengenezo ya barabara, madaraja, makaravati na mifereji ya maji, pamoja na kuandaa wakandarasi na wataalamu watakaoweza kuchukua hatua kwa haraka pale dharura itakapotokea. Aidha, ametaja kuwa baadhi ya miundombinu iliyowekwa ni makaravati ya kupitisha maji, makaravati ya plastiki aina ya HDPE pamoja na gabions, kwa lengo la kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na maji ya mvua.
Hata hivyo TANROADS imefanya pia utambuzi na tathmini ya maeneo hatarishi (prone areas) yanayotarajiwa kuathiriwa zaidi na mvua kubwa na mafuriko. Maeneo hayo yanahusisha mabonde, maeneo yenye mifereji ya maji, maeneo yaliyo karibu na madaraja na makaravati, pamoja na maeneo ambayo yana historia ya kukatika, kusombwa au kuharibika kwa barabara wakati wa mvua kubwa.
Maeneo hayo tayari yametembelewa na Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Kagera, iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Kido, kwa ajili ya kutathmini hali halisi na kuweka mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza wakati wa mvua hizo.
TANROADS pia imeeleza kuwa gharama za maandalizi na utekelezaji wa hatua mbalimbali za kukabiliana na athari za mvua za El Niño zinakadiriwa kufikia shilingi bilioni 6.7, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha miundombinu ya barabara inaendelea kuwa salama na kupitika wakati wa mvua.
Mhandisi Christian Mbise amewataka madereva na watumiaji wote wa barabara kuwa waangalifu, hasa wakati wa mvua kubwa, kupunguza mwendo, kufuata alama na maelekezo ya usalama barabarani na kuepuka kulazimisha kupita katika maeneo ambayo barabara au madaraja yameathiriwa na maji.
Aidha, wananchi wametakiwa kutoa taarifa mapema wanapoona miundombinu ya barabara, madaraja, makaravati au maeneo mengine yakiwa katika hali hatarishi, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa na kupunguza uwezekano wa madhara kwa maisha na mali.
TANROADS imesema itaendelea kufanya ufuatiliaji na matengenezo ya miundombinu kwa kushirikiana na mamlaka nyingine za serikali na wananchi ili kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara wakati wote wa msimu wa mvua.



