Na Mwandishi wetu, Urithi Geopark Karatu

Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Mhe. Dkt. Lameck Karanga, ameipongeza Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kufuatia jitihada zinazofanywa na Mamlaka hiyo kutumia teknolojia za kidijitali kutangaza maajabu ya vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro ambapo matumizi ya teknolojia hiyo yanasaidia kuwaita watalii mbalimbali duniani.

Dkt. Karanga alitoa pongezi hiyo tarehe 27 Septemba, 2026, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yaliyofanyika katika jengo la Makumbusho ya Urithi Geopark, Wilayani Karatu mkoani Arusha yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “ Ajenda ya Kidijitali na Akili Bandia katika Kubuni upya Utalii,”

Mhe. Karanga ameongeza kuwa matumizi ya teknolojia katika utalii yamekuwa muhimu katika kuwafikia watalii kwa urahisi zaidi, hususan katika kipindi ambacho teknolojia imekuwa sehemu ya maisha ya kila siku. 

“Tunapoadhimisha siku hii tumepata nafasi ya kujionea jinsi ambavyo Ngorongoro mnatumia teknolojia kutangaza vivutio vya utalii, pamoja na vitu vingine tumeona matumizi ya QR codes kupata taarifa za vivutio vya utalii, tumeona matumizi ya Visual reality ambayo ni jitihada kubwa ya mapinduzi ya kutangaza utalii kisasa” ,alisema Dk. Karanga 

Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Joas Makwati, amebainisha kuwa Ngorongoro inaendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kutangaza utalii wa wanyamapori, malikale, urithi wa utamaduni, jiolojia, kuibua mazao mapya ya utalii sambamba na kuboresha huduma kwa wateja kupitia miumo wa kisasa wa malipo na kuingia na kutoka ndani ya hifadhi wa Vipenyo Smart Gates (VGS).

Ngorongoro imefanya maadhimisho hayo kwa kushirikisha wadau kufanya mbio fupi (Fun Run) na michezo kwa lengo la kuhamasisha jamii kushiriki katika shughuli za utalii na michezo, pamoja na kuelimisha kuhusu umuhimu wa utalii katika kuchochea maendeleo ya jamii.