NA DENIS MLOWE, IRINGA

MBUNGE wa Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, Ritah Kabati, amefika katika Shule ya Sekondari Ilole na kutoa msaada kwa wanafunzi, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni sehemu ya jitihada zake za kuwaunga mkono vijana na kuchangia katika kuboresha mazingira ya elimu.

Akizungumza wakati wa kupokea msaada huo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ilole, Sai alimshukuru Mbunge Kabati kwa kuendelea kuonesha kujali mahitaji ya wanafunzi na shule hiyo.

Sai alisema Kabati amekuwa akiwafikia wananchi na vijana katika maeneo mbalimbali ya Jimbo la Kilolo na kusaidia pale anapobaini changamoto zinazohitaji ushirikiano.

Alisema pia Mbunge huyo amekuwa akishiriki katika shughuli za maendeleo ya shule hiyo, akitoa mfano wa msaada wa Sh milioni 16 alioutoa hivi karibuni kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa bweni la wasichana linalojengwa kwa nguvu za wananchi.

“Kwa niaba ya walimu wenzangu, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge kwa msaada ambao ametupatia. Amekuwa msaada mkubwa kwetu na hasa kwa vijana wetu ambao wana mahitaji mbalimbali,” alisema Sai.

Aidha, Sai alimuomba Mungu aendelee kumbariki Mbunge Kabati na kumpa nguvu zaidi katika kutekeleza majukumu yake ya kuwahudumia wananchi.

Kwa upande wake, mwanafunzi wa Kidato cha Nne na kiongozi wa michezo katika Shule ya Sekondari Ilole, Rehama Mfikwa, alimshukuru Mbunge Kabati kwa msaada alioutoa kwa wanafunzi.

Mfikwa alisema msaada huo umewapa faraja na kuwaongezea hamasa ya kuendelea kujituma katika masomo na michezo.

“Tunaishukuru sana Mbunge wetu mama Ritah Kabati kwa kutusaidia na kutuonesha kwamba anatupenda na kutujali. Tunamuomba Mungu aendelee kumbariki na kuongeza nguvu ili aendelee kuwasaidia vijana wenye mahitaji,” alisema Mfikwa.

Akizungumza na wanafunzi hao, Kabati aliwataka kutumia msaada walioupata kwa malengo yaliyokusudiwa na kuhakikisha unawasaidia kuboresha masomo yao na maisha yao kwa ujumla.

Aliwataka wanafunzi kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kuheshimu walimu, wazazi na walezi, akisisitiza kuwa elimu ndiyo msingi muhimu wa kufikia ndoto zao.

Kabati pia aliwataka vijana kutokata tamaa wanapokutana na changamoto za maisha, bali wajifunze kuzitumia changamoto hizo kama sehemu ya kujijenga na kufikia malengo yao.

“Nataka muweke mbele elimu, nidhamu na kujituma. Msiache changamoto ziwafanye mkate tamaa. Tumia kila fursa mnayoipata kujijenga, kwa sababu Taifa linawahitaji vijana wenye elimu, maarifa, nidhamu na uzalendo,” alisema Kabati.

Aidha, aliwataka wanafunzi kutumia vizuri muda wao, kujiepusha na makundi yasiyofaa na kuzingatia masomo pamoja na vipaji walivyonavyo katika michezo na shughuli nyingine za kujenga maisha yao.

Kabati alisema ataendelea kushirikiana na wananchi na taasisi mbalimbali katika kuunga mkono juhudi za kuboresha elimu na kuwawezesha vijana katika Jimbo la Kilolo.