Waziri wa Katiba na Sheria DKT Juma Homera,akikabidhi fedha Kiasi cha Shilingi milioni 1 kwa Afisa Mtendaji Kijiji cha Likuyumandela Emanuela Ngulu kwa ajili ya kuboresha Huduma za afya.
Baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya Likuyu kinachojengwa na Kampuni ya Mantra Tanzania Ltd.
Na Muhidin Amri, Namtumbo
ZAIDI ya wakazi 13,005 wa kata ya Likuyusekamaganga wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma,wanatarajiwa kupata huduma za afya baada ya Kampuni ya Mantra Tanzania Ltd inayojishughulisha na utafiti wa madini ya Uraniam katika mto Mkuju kuwa katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa kituo kipya cha afya.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo Meneja Mahusiano wa Mantra Manase Ndoroma alisema,wamekamilisha kujenga majengo ya kutolea huduma na kazi zinazoendelea kwa sasa ni ujenzi wa nyumba mbili za watumishi ambazo zitawawezesha wataalam hao kuishi karibu na eneo la kazi.
Alisema,lengo ni kuhakikisha kituo hicho kinaanza kutoa huduma kwa wananchi ambao wanalazimika kwenda maeneo mengine ikiwemo Hospitali ya wilaya Namtumbo mjini kufuata matibabu.
Alisema mwaka 2026/2027 wataendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi mbalimbali ili kuwawezesha kuwa na afya na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
“Mheshimiwa Waziri, baada ya kukamilisha kujenga majengo ya kutolea huduma,tumeanza na ujenzi wa mnara wa kuweka tenki la kuhifadhi maji,tunajenga vyoo vitano vya kisasa na kati ya hivyo,viwili kwa ajili ya wanaume,viwili vya wanawake na kimoja cha watu wenye ulemavu pamoja sehemu ya kunawia mikono,mashimo ya taka nyepesi na ngumu na ujenzi wa nyumba ya walimu katika shule ya msingi Muungano”alisema Manase.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Juma Homera,ameupongeza uongozi wa Mantra Tanzania Ltd kuisaidia Serikali katika kuboresha huduma za afya, na amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kampuni hiyo ili miradi yote ikamilike haraka.
Dkt Homera alisema,mradi huo ni kupunguza msongamano katika vituo vingine vya afya vilivyopo,kupunguza gharama na muda wa kusafiri kufuata matibabu pamoja na kuimarisha huduma za kinga na tiba kwa wananchi.
Alisema,kituo kitakapokamilika kitaongeza ubora wa huduma za afya,kuokoa maisha ya wananchi kwa kuwafikishia huduma kwa wakati na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kata ya Likuyu na meneo jirani.
