Na. Mwandishi wetu, RUVUMA
Wakulima mkoani Ruvuma wanatarajiwa kunufaika na matumizi ya Kadi Janja za Mkulima, zinazolenga kurahisisha utambuzi wao pamoja na upatikanaji wa huduma za pembejeo na kifedha kupitia mifumo ya kidijitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi kadi hizo kwa wakulima mwishoni mwa wiki, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya alisema zoezi hilo ni utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya Kilimo ya kuhakikisha wakulima wote nchini wanatambuliwa katika mifumo ya kidijitali.
“Tupo hapa Mkoani Ruvuma kutekeleza maelekezo ya Wizara ya Kilimo kuwa wakulima wa nchi hii watambuliwe katika mifumo ya kidijitali. Leo hii, tukishirikiana na wenzetu wa CRDB na BizTech tupo kuwakabidhi wakulima Kadi Janja ambazo zitakuwa utambulisho wao,” alisema Ng’ondya.
Aliongeza kuwa kadi hizo zimeunganishwa na taarifa muhimu za mkulima, ikiwemo ukubwa wa mashamba na namba ya akaunti ya CRDB, ili kuwawezesha kufanya miamala kwa njia ya kidijitali.
Kwa upande wake, Meneja wa Bidhaa za Kadi wa Benki ya CRDB, Daniel Mugwagi alisema mwaka 2025 benki hiyo ilikusanya taarifa za wakulima na kuwezesha utengenezaji wa kadi hizo huku pia wakiwa wametengeneza mfumo utakaotumiwa na wauzaji wa pembejeo kwa kuwapatia mashine maalumu za kutoa huduma kwa wakulima wanaonunua mbolea ya ruzuku.
Katika hatua nyingine, Afisa Mkuu wa Biashara kutoka Kampuni ya BizTech, Kelvin Masai alisema kampuni hiyo imeungana na washirika wake kuhakikisha mkulima ananufaika na mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya kilimo kupitia teknolojia ya programu tumizi itakayowawezesha wauzaji wa pembejeo kusimamia biashara zao za uuzaji wa mbolea ya ruzuku na kutunza taarifa muhimu za biashara na wakulima.

