Happy Lazaro,Arusha .

Arusha.Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amesema kuwa ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi wa barabara kutoka Usa River hadi Maji ya chai mkoani Arusha.

Ameyasema hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kipande cha barabara kutoka Usa River hadi Maji ya Chai, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo.

Dkt. Msonde amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha kazi zinaendelea kwa kasi na kukamilika kwa wakati, huku viwango vya ujenzi vikizingatiwa.

Naye Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema hatua mbalimbali zimechukuliwa kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Besta amesema usimamizi wa karibu wa mradi ni muhimu ili kuhakikisha kasi ya ujenzi inaendana na ubora wa kazi zinazotekelezwa.

Besta amesema kuwa, hatua ya kuwashirikisha wakandarasi kadhaa katika utekelezaji wa mradi huo inalenga kuongeza kasi ya ujenzi na kuhakikisha kazi zinafanyika kwa wakati katika maeneo mbalimbali ya mradi.

Naye Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha, Reginald Massawe, ametoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo, akieleza hatua mbalimbali ambazo zimefikiwa pamoja na mikakati inayotekelezwa kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Massawe amesema TANROADS inaendelea kusimamia utekelezaji wa kazi hizo kwa karibu, ikiwemo kuhakikisha wakandarasi wanafuata ratiba na viwango vilivyowekwa.

Kwa upande wao wananchi ,akiwemo Dickson Mungure wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na barabara ya Usa River hadi Kilimanjaro International Airport (KIA), wameeleza faraja yao kutokana na kasi ya ujenzi wa barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami.

Wananchi hao wamesema kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, huku kukitarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi kwa wakazi wa maeneo yanayopitiwa na barabara hiyo.

Wamesema barabara bora itarahisisha usafiri wa watu na bidhaa, kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa safari na kutoa mazingira bora zaidi kwa wafanyabiashara na shughuli nyingine za kiuchumi.

“Barabara hiyo inatarajiwa kuwa na umuhimu katika kuimarisha muunganiko wa maeneo ya Arusha na miundombinu muhimu ya usafiri, ikiwemo uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.”wamesema wananchi hao.