Ujumbe wa Vietnam ukiongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo na Mazingira wa nchi hiyo, Mhe. Nguyen Hoang Hiep, umetembelea Septemba 25, 2026 shamba la misitu la Serikali lililopo Arusha, linalosimamiwa na Mhifadhi wa Misitu, Bw. Ernest Madatta. 

Lengo ziara ya ujumbe huo kwenye shamba hilo lilikuwa ni kujifunza kuhusu usimamizi wa misitu, uhifadhi wa mazingira na fursa za utalii ikolojia.

Shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 8,170 lilianzishwa mwaka 1920 chini ya Tangazo la Serikali Na. 232, huku takribani hekta 6,550 zikiwa zimepandwa miti ya kigeni, hususan aina ya Pinus patula. Shamba hilo, lililopo takribani kilomita 20 kutoka Jiji la Arusha karibu na Mlima Meru, huzalisha miche kwa ajili ya kupandwa na kutoa malighafi kwa mahitaji ya soko la ndani, sambamba na kuhifadhi udongo, maji na bioanuwai.

Aidha, shamba hilo linachangia ulinzi wa vyanzo vya maji, ajira kwa jamii inayolizunguka na shughuli za utalii ikolojia kupitia maporomoko ya maji, wanyama wadogo na ndege. Pia, linaendesha shughuli za ufugaji nyuki na uzalishaji wa asali kwa ajili ya jamii, huku likianza kwa kiwango kidogo ukusanyaji wa utomvu wa miti aina ya Pinus patula.

Kwa upande wake, Naibu Waziri, Mhe. Nguyen Hoang Hiep amepongeza juhudi za Serikali katika usimamizi na uhifadhi wa shamba hilo, akieleza kuwa Vietnam pia ina uzoefu wa misitu inayosimamiwa na Serikali na inaendelea kuendeleza uhifadhi wa misitu pamoja na utalii ikolojia.

Ujumbe huo pia ulishiriki Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Vietnam uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 21 hadi 23 Septemba, 2026