NA MWANDISHI WETU
SERIKALI imeishukuru Benki ya NMB kwa kuendelea kudhamini Tamasha la Kariakoo ‘Kariakoo Festival 2026’, huku ikiipongeza kwa Huduma na Bidhaa Bunifu zinazochochea ukuaji kiuchumi miongoni mwa wafanyabiashara nchini, zikiwemo NMB SME’s Credit Card na Mshiko Fasta.
Shukrani na pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, wakati akizindua msimu wa tatu wa Kariakoo Festival 2026, jukwaa la linalowakutanisha wafanyabiashara na wanunuzi wa ndani na nje, likiratibiwa na Kampuni ya One Voice Events na kudhaminiwa na Benki ya NMB.
Kariakoo Festival 2026 imezinduliwa Ijumaa Septemba 25 na jukwaa hilo litafanyika hadi Septemba 27, ambapo Naibu Waziri Londo amewataka washiriki kulitumia vema kufanikisha safari ya mabadiliko ya kisekta kuelekea Uchumi Usiotegemea Pesa Taslimu (cashless economy).
Mkuu wa Idara ya Biashara ya NMB, Alex Mgeni, alisema kupitia jukwaa la Kariakoo Festival, benki yake imezileta huduma bora na rafiki kwa wafanyabiashara na wajasiriamali, ikiwemo SME’s Credit Card, NMB Mkononi, NMB Tap to Pay, NMB Lipa Namba na Mshiko Fasta.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara wa Kariakoo (JWK), Severine Mushi, naye aliishukuru Serikali kwa kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara nchini, kiasi cha kuzivutia taasisi za fedha kama NMB, kuwekeza kufanikisha matukio yanayowakutanisha wadau wa biashara kitaifa na kimataifa.

