Na Mwandishi wetu, Geita

MKUU wa Mkoa wa Geita Alexander Pastory Mnyeti amesema maonyesho ya tisa ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanatarajiwa kuzinduliwa kesho Septemba 27 mwaka 2026 na Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ally Mwinyi na yanatarajiwa kufungwa Oktoba 3, mwaka 2026 na Waziri Mkuu, Dkt Mwigulu Lameck Nchemba.

RC Mnyeti akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 26, 2026 amesema maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya ufunguzi na kauli mbiu ya maonesho hayo ni “Madini ni Utajiri, Tuwajibike kwa Pamoja Kufikia Dira ya Taifa 2050.”

Mkuu huyo wa mkoa amesema maonesho hayo yanakutanisha washiriki 765 kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi, wakiwamo wachimbaji, wajasiriamali, taasisi za fedha na wauzaji wa teknolojia na vifaa vya uchimbaji huku mataifa tisa yakishiriki.

RC Mnyeti amesema washiriki hao wanatoka katika maeneo mbalimbali chini ya mnyororo wa thamani wa madini na sekta zinazofungamana na uchimbaji.

Amesema washiriki hao ni pamoja na kampuni 15 za uchimbaji madini, taasisi 41 za umma, wajasiriamali 599, wachimbaji wadogo, vijana na watu wenye mahitaji maalum 52, taasisi saba za fedha na kampuni 11 zinazouza vifaa vya utafiti na uchimbaji.

Pia wapo watoa huduma mbalimbali, wakiwamo watoa huduma za vyakula na vinywaji 29, kampuni tano za ulinzi, watoa huduma watano wa michezo na burudani kwa watoto pamoja na mwakilishi mmoja kutoka sekta ya wanyamapori.

“Maonesho haya yamekusudia kuwaunganisha wadau wote katika mnyororo wa thamani wa madini, wakiwamo wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa teknolojia pamoja na wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini,” amesema RC Mnyeti.

RC Mnyeti amesema maonesho hayo yanalenga kuongeza matumizi ya teknolojia katika shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini nchini, pamoja na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika pato la taifa.

Malengo mengine ni kukuza matumizi sahihi ya teknolojia katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kuwaunganisha wachimbaji na taasisi za Serikali, wizara, wadau wa madini na taasisi wezeshi, pamoja na kuwaunganisha wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo ili kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

Lengo lingine ni kuwaunganisha wafanyabiashara wanaofanya shughuli katika mnyororo wa thamani wa madini na sekta zinazofungamana na madini.Maonesho hayo pia yanalenga kuifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa maonesho bora ya teknolojia ya madini na sekta fungamanishi barani Afrika ifikapo mwaka 2035.