Na John Mapepele– New York

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema uwekezaji unaofanywa na Serikali Dkt. Samia Suluhu Hassan umeiwezesha Tanzania kuimarisha huduma za afya ya mama na mtoto, pia kusogeza huduma za dharura za uzazi na watoto wachanga karibu zaidi na wananchi huku mataifa mbalimbali wakipongeza kwa hatua hiyo.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo Septemba 24, 2026 jijini New York, Marekani wakati akimkaribisha Makamu wa Rais Mhe.Deogratius Njedembi azungumze kwa niaba ya Mhe. Rais Samia wakati wa mkutano uliofanyika pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa (UNGA 2026),

Mgeni rasmi wa mkutano huo Rais wa Namibia Mhe.Netumbo Nandi-Ndaitwah alimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa aliyoifanya katika eneo la mama na mtoto na kumhakikishia kuwa kwa kazi nzuri inayofanyika Namibia itaendelea kuwa bega kwa bega na Tanzania.

Rais na Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na Afya la Jihpiego Dkt. Allyson Bear katika majadiliano amepongeza Rais Samia kwa mikakati mizuri ya kuokoa maisha ya watoto wachanga na akina mama huku akizitaka nchi nyingine kuiga kwa Tanzania

Aidha, Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa mafanikio hayo yamechangiwa na dhamira ya kisiasa, uwekezaji katika mifumo ya afya pamoja na kuimarishwa kwa huduma zinazolenga kuokoa maisha ya akina mama na watoto.

Amesema juhudi hizo zilianza kupewa msukumo mkubwa mwaka 2018 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akiwa Makamu wa Rais, alipoanzisha kampeni ya “Jiongeze Tuwavushe Salama” iliyohamasisha viongozi na wadau kuongeza juhudi na rasilimali katika kuhakikisha akina mama wanapata huduma salama wakati wa ujauzito na kujifungua.

“Haikuwa kaulimbiu tu, ilikuwa ni uhamasishaji wa dhamira na rasilimali na ndiyo iliyoweka msingi wa mafanikio tunayoyaona leo, Serikali imeendelea kuwekeza katika watu na mifumo kwa kukarabati vituo vya afya, kutoa mafunzo na kusambaza watumishi wa afya, kuboresha upatikanaji wa dawa pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa utendaji.” Amesema Mhe. Mchengerwa

Mhe. Mchengerwa amesema huduma za watoto wachanga zimeendelea kusogezwa kutoka hospitali za rufaa hadi katika vituo vya afya ya msingi, hatua inayowezesha watoto wengi zaidi kupata huduma muhimu karibu na maeneo wanayoishi, huku maendeleo ya huduma hizo yakiwezesha hata baadhi ya watoto wanaozaliwa na uzito mdogo wa gramu 500 hadi 700 kupata huduma na kuendelea kuishi.

Amefafanua kuwa mageuzi hayo yanaenda sambamba na azma ya Tanzania kuwa kitovu cha huduma za kibingwa za afya katika ukanda wa Afrika, ambapo huduma kama upasuaji wa moyo, upandikizaji wa uboho katika Hospitali ya Benjamin Mkapa na upandikizaji wa vifaa vya kusaidia kusikia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili zimeendelea kuvutia wagonjwa kutoka nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini.

Aidha, amesema mafanikio hayo yanaonesha kuwa utashi wa kisiasa, uelewa wa mazingira ya kijamii na kiutamaduni pamoja na uwekezaji katika mifumo ya afya vinaweza kuleta matokeo makubwa katika kuokoa maisha ya wananchi, huku akisisitiza dhamira ya Tanzania kuendelea kuunga mkono ajenda ya “Zero Tatu” inayolenga kutokuwepo kwa uzazi wa nyumbani, vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na watoto wachanga pamoja na watoto ambao hawajapata chanjo.