Na Ssgt Mawazo Mtondo – MWANZA

Timu ya mpira wa wavu wanaume ya Jeshi la Magereza 25 Septemba, 2026 imepata ushindi wa kusisimua wa seti 3–2 dhidi ya Timu ya Ngome ya JWTZ, katika mchezo mkali na wa kuvutia wa Mashindano ya Bammata 2026 yanayoendelea Jijini Mwanza.

Mchezo huo uliokuwa na mashambulizi makali, ulinzi imara na mabadiliko ya kasi ya mchezo, uliifanya kila timu kupigania kila pointi. Magereza ilionyesha uthubutu na umakini hadi hatua za mwisho na hatimaye kuibuka na ushindi huo wa muhimu, uliowapa wachezaji morali na hamasa zaidi kuelekea michezo inayofuata.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ssgt Mussa Shabani, amesema ushindi huo umetokana na umoja, nidhamu, kujituma na kupambana kwa wachezaji, huku akisisitiza kuwa timu itaendelea kuongeza nguvu na kuboresha maeneo yaliyobainika katika mchezo huo.

Naye Kapteni wa timu hiyo, Wdr Martin Anthony, amesema ushindi huo umeongeza morali ndani ya kikosi na kwamba wachezaji wataendelea kupambana kwa moyo, nguvu na mshikamano, wakilenga kufanya vizuri katika michezo iliyosalia ya mashindano hayo.