Na Oscar Assenga, TANGA
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, ameipongeza CCM Mkoa wa Tanga kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 36 za watumishi wake wenye thamani ya Sh2.5 bilioni.
Nyumba hizo zinajengwa katika wilaya zote tisa za Mkoa wa Tanga, ambapo kila wilaya inatarajiwa kupata nyumba nne kwa ajili ya kuboresha mazingira ya makazi na utendaji wa viongozi na watumishi wa chama hicho.
Kihongosi alitoa pongezi hizo alipofanya ukaguzi wa maendeleo ya mradi huo katika ziara yake ya siku mbili mkoani Tanga, akisema uimarishaji wa miundombinu ya chama ni sehemu muhimu ya kuweka mazingira bora ya utekelezaji wa majukumu.
Alisema uwepo wa miundombinu na mazingira mazuri ya kazi ni muhimu katika kuhakikisha viongozi na watumishi wa CCM wanatekeleza majukumu yao kwa ufanisi katika ngazi zote.
“Utekelezaji wa Ilani ya CCM unahitaji pia mazingira bora ya kazi na miundombinu inayowezesha shughuli za chama kufanyika kwa ufanisi,” alisema Kihongosi.
Alisema ujenzi wa nyumba hizo unaendana na maelekezo ya chama ya kuimarisha miundombinu yake, hatua ambayo itasaidia kuboresha mazingira ya kazi na makazi kwa watumishi katika ngazi za wilaya.
Kihongosi yupo mkoani Tanga kwa ziara ya siku mbili kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM pamoja na shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na chama hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tanga Rajab Abdurhaman alisema tayari ametenga Sh1 bilioni kwa ajili ya kuwezesha na kuharakisha ujenzi wa nyumba hizo.
Alisema mradi huo unatarajiwa kukamilika Februari mwakani na kwamba utakapo kamilika utasaidia kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa viongozi na watumishi wa chama katika maeneo mbalimbali ya mkoa.
Kwa mujibu wa mpango wa ujenzi huo, kila wilaya kati ya wilaya tisa za Mkoa wa Tanga itapata nyumba nne, ambazo zitatumika kama makazi ya watumishi wa CCM katika ngazi hizo.

