Mwenyekiti Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo Taifa, Ndugu Juma Duni Haji, jana Septemba 24, 2026, alifika nyumbani kwa familia ya Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mzee Amani Abeid Karume, kutoa mkono wa pole kufuatia msiba wa kuondokewa na mama yao mpendwa, Bi. Fatma Karume.
Katika ziara hiyo, Babu Duni aliambatana na viongozi mbalimbali, akiwemo Naibu Katibu Mkuu Mstaafu wa ACT Wazalendo, Nassor Ahmed Mazrui, pamoja na Sheikh Bakar Haji Muhammad kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Babu Duni amesema msiba wa Bi. Fatma Karume ni wa wote, ingawa baadhi ya watu wameguswa zaidi kutokana na ukaribu wao na marehemu.
Aidha, alimuombea dua marehemu Bi. Fatma Karume, akimwomba Mwenyezi Mungu amsamehe makosa yake na amlaze mahala pema peponi, Jannatul-Firdausi.
Vilevile, aliwaombea wafiwa kwa Mwenyezi Mungu awape subira na nguvu katika kipindi hiki cha maombolezo.
Chama cha ACT Wazalendo kimeendelea kuungana na familia ya Mzee Amani Abeid Karume katika kipindi hiki cha maombolezo, huku kikitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na wote walioguswa na msiba huo.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu Bi. Fatma Karume mahala pema peponi. Amina.

