Na. OWM (KAM), Dar es Salaam
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Dkt. Evaline Munisi, amepongeza Kanisa la Waadventista wa Sabato Salasala (SDA) kwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha mshikamano wa kijamii, kukuza maadili ya uadilifu, uwajibikaji na upendo, pamoja na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani na mshikamano wa kitaifa.
Mhe. Dkt. Munisi amesema hayo leo, Septemba 26, 2026, katika harambee ya kuchangia ujenzi na maendeleo ya Kanisa la Waadventista wa Sabato (SDA), Salasala, jijini Dar es Salaam.
Amesema, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano imejipanga kushirikiana na makundi ya kijamii katika kudumisha mshikamano, kukuza ustahimilivu, kuimarisha maadili ya kazi na kusaidia jitihada za kijamii na maendeleo endelevu.
Kadhalika, Dkt. Munisi amewapongeza viongozi na waumini wa Kanisa la SDA Salasala kwa kuandaa harambee hii ya ujenzi wa kanisa yenye lengo la kukusanya Shilingi milioni 400 kwa ajili ya kujenga jamii imara.
“Tusimame pamoja, tutoe kwa moyo wa furaha, tutashuhudia Kanisa la Waadventista wa Sabato linajengwa na kudumishwa imara kwa utukufu wa Mungu,” amesema Dkt. Munisi.
Vilevile, Dkt. Munisi amewasihi viongozi na waumini wa kanisa kuendelea kuyaenzi na kuimarisha mafundisho ya kiroho na malezi ya watoto na vijana, umoja, upendo na mshikamano, ushirikiano na Serikali, pamoja na kuwa na uwazi, uwajibikaji na usimamizi madhubuti wa rasilimali za kanisa.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Majengo, Bw. Charles Wangwe kutoka Kanisa la SDA Salasala, ameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha, kulinda na kudumisha amani, utulivu, umoja na mshikamano na mahusiano mema miongoni mwa Watanzania wa makundi ya imani mbalimbali katika Taifa letu.
Ameendelea kwa kusema kuwa kanisa linaendesha hospitali, kliniki, vituo vya afya na zahanati katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo Zahanati ya Pemba, vituo 12 vya afya, ambazo ni zahanati 11 na polyclinic moja.
Sambamba na hayo, Kanisa la Waadventista wa Sabato limekuwa likichangia katika maendeleo ya elimu, ambapo jumla ya shule 27 za awali, 23 za msingi, 18 za sekondari, Chuo kimoja cha VETA, Chuo kimoja cha Afya na Chuo kimoja cha kati kilichopo Dodoma.
Amesema Kanisa la Waadventista wa Sabato lilianzishwa mwaka 2007 likiwa na washiriki wachache; mwaka 2010 washiriki walifika 150, mwaka 2018 waumini 400 na wengine kukaa nje, jambo lililosababisha kuanzishwa kwa ujenzi wa jengo kubwa lenye uwezo wa kuchukua watu 1,500 na kukadiriwa kugharimu Shilingi bilioni 3.

