Na Fullshangwe Media 

WANANCHI wa Kata ya Ndungu, Jimbo la Same Mashariki, Wilaya ya Same, Mkoa wa Kilimanjaro, wameangua kilio mbele ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, wakieleza namna ukosefu wa huduma ya maji safi na salama unavyowaathiri.

Wananchi hao wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, hali inayowalazimu kutumia maji yasiyo salama kwa matumizi ya binadamu na hivyo kuongeza hofu kuhusu afya zao.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Jana tarehe 24/9/2026 Kata ya Ndungu, mbele ya Naibu Katibu Mkuu huyo, wananchi walisema eneo hilo halina miundombinu ya kutosha ya maji, licha ya changamoto hiyo kuendelea kwa muda mrefu bila kupata ufumbuzi wa kudumu.

Walisema wamekuwa wakifikisha kilio chao kwa viongozi mbalimbali waliowahi kutembelea kata hiyo, lakini hadi sasa hawajaona suluhisho la kudumu la tatizo hilo.

Diwani wa Kata ya Ndungu alisema changamoto ya maji imekuwa ni tatizo kubwa kwa wananchi, akieleza kuwa wamekuwa wakitoa kilio hicho mara kwa mara kwa viongozi mbalimbali bila kupata majibu ya uhakika kuhusu lini tatizo hilo litapatiwa ufumbuzi.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao walimuomba Naibu Katibu Mkuu huyo kusaidia kufikisha kilio chao kwa Serikali ili hatua zichukuliwe za kuhakikisha wanapata huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, Aggrey Mwanri, alikiri kupokea na kuelewa changamoto hiyo, akisema atawasilisha suala hilo kwa Waziri wa Maji, Juma Aweso, ili hatua za kulitatua ziweze kuchukuliwa.

Mwanri alisema changamoto hiyo inahitaji kufanyiwa kazi ili wananchi wa Ndungu waweze kupata huduma ya maji safi na salama, huku akieleza kuwa atahakikisha kilio hicho kinawafikia wahusika katika Serikali kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi.