Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amekutana na ujumbe wa Vietnam Septemba 25, 2026 ulioongozwa na Naibu Waziri wa Kilimo na Mazingira, Mhe. Nguyen Hoang Hiep, walipomtembelea katika Ofisini kwake kwa lengo la kujadili fursa za kuimarisha ushirikiano na kuongeza biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Vietnam.
CPA Makalla ameukaribisha ujumbe huo Arusha na kueleza utayari wa Mkoa huo kushirikiana na Vietnam katika kuwezesha uwekezaji na shughuli nyingine za maendeleo.
Aidha, amepongeza mchango wa Vietnam katika sekta ya mawasiliano nchini kupitia Kampuni ya Halotel, akieleza kuwa ushirikiano huo unaonesha fursa zilizopo kati ya nchi hizo mbili.
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Nguyen Hoang Hiep ameeleza fursa za kuimarisha biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi, akitaja sekta ya mifugo kuwa miongoni mwa maeneo yenye fursa Arusha.
Aidha, ameeleza kuwa Vietnam inalenga kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania kupitia juhudi za pamoja za utangazaji na kukuza vivutio vya utalii vilivyopo Arusha.
Ujumbe wa Vietnam mbali na kutembelea Arusha, pia ulishiriki mkutano wa Pili wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na nchi hiyo, uliofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 21 hadi 23 Septemba, 2026.

