Kahama, Septemba 24, 2026 – Wakazi na wafanyabiashara wa Kahama mkoani Shinyanga wanatarajiwa kunufaika na upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kifedha kwa urahisi zaidi, kufuatia Yas Tanzania kufungua duka jipya mjini humo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa duka hilo, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mhe. Mataluma Kaniki alisema kuendelea kuongezeka kwa uwekezaji wa sekta binafsi ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira katika Manispaa hiyo.
“Kahama ni miongoni mwa maeneo yanayokua kwa kasi kiuchumi kutokana na shughuli za madini, kilimo na biashara. Tunapopata uwekezaji kama huu, tunaona matokeo yake si katika huduma pekee, bali pia katika ajira, biashara zinazozunguka uwekezaji huo na mchango wake katika uchumi wa Manispaa yetu. Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri yatakayovutia uwekezaji zaidi Kahama,” alisema Mhe. Kaniki.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja na Uendeshaji wa Yas Tanzania, Bi. Mwangaza Matotola, alisema duka hilo limefunguliwa ili kuwapa wateja wa Kahama sehemu ya kupata huduma na msaada wanaouhitaji kwa urahisi zaidi.
“Tunataka mteja wa Kahama apate huduma anayoihitaji kwa urahisi na kwa wakati. Duka hili linatupa nafasi ya kuwa karibu zaidi na wateja wetu, kusikiliza mahitaji yao, kutatua changamoto zao na kuwapatia huduma za Yas na Mixx katika sehemu moja,” alisema Matotola.
Alisema duka hilo ni sehemu ya mtandao wa zaidi ya maduka 556 ya Yas nchini, yanayowezesha wateja kupata huduma mbalimbali ikiwemo za laini, intaneti, vifaa vya mawasiliano na huduma za kifedha.
Matotola alisema upanuzi wa maduka unaenda sambamba na uwekezaji wa zaidi ya Sh trilioni moja ambao Yas imefanya katika kupanua na kuboresha miundombinu na huduma zake nchini.
Kwa mujibu wake, Yas kwa sasa ina zaidi ya minara 4,900, inayowezesha huduma za teknolojia za 4G na 5G katika maeneo mbalimbali, huku ikihudumia zaidi ya wateja milioni 33.2 Tanzania Bara na visiwani.
Alisema uwekezaji katika mtandao na vituo vya huduma kwa wateja unalenga kuhakikisha ongezeko la matumizi ya huduma za kidijitali linaenda sambamba na upatikanaji wa msaada wa moja kwa moja kwa wateja.
“Kadiri matumizi ya teknolojia yanavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya wateja yanavyobadilika. Ndiyo maana tunaendelea kuwekeza si tu kwenye mtandao, bali pia kwenye maeneo ambayo mteja anaweza kufika, kuzungumza nasi na kupata suluhisho la mahitaji yake,” alisema Matotola.
Mbali na kusogeza huduma karibu na wateja, kufunguliwa kwa duka hilo kumeongeza pia fursa za ajira kwa vijana wa Kahama, ikiwa ni sehemu ya manufaa ya uwekezaji huo kwa jamii.

