Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma.
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema migogoro ya ardhi imekuwa miongoni mwa kero kubwa zinazowasilishwa na wananchi, huku Serikali ikipanga kupitia upya mfumo wa mabaraza ya ardhi ili kuongeza ufanisi katika utatuzi wa migogoro hiyo.
Ameyasema hayo Septemba 25, 2026, Mtumba jijini Dodoma, wakati akizungumza katika Programu Maalumu ya Sema na Waziri, ambapo amesema Serikali inaangalia namna ya kuyaongezea nguvu mabaraza ya ardhi ya vijiji, kata na wilaya ili yaweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kushughulikia migogoro kabla haijafikia hatua za mahakamani.
Amesema kwa sasa mabaraza hayo yana nafasi kubwa katika usuluhishi, lakini Serikali inaendelea kutathmini iwapo yataongezewa mamlaka au baadhi ya majukumu yao kuhusishwa zaidi na mfumo wa mahakama, hatua ambayo amesema inalenga kuhakikisha mashauri ya ardhi yanamalizika kwa wakati na wananchi wanapata haki.
Aidha, Dkt. Homera amesema suala hilo linakwenda sambamba na maelekezo ya Serikali kuhusu kupunguza migogoro ya ardhi pamoja na migogoro kati ya wakulima na wafugaji, akieleza kuwa Wizara yake itashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika hatua za kuboresha sheria zinazohusika.
Akizungumzia malalamiko ya baadhi ya wananchi kutolewa mali zao nje katika migogoro ya umiliki wa nyumba, Dkt. Homera amesema suala hilo linahitaji kufuatiliwa kwa kina kwa kuwa mazingira ya kila tukio yanaweza kutofautiana, na kwamba atawasiliana na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Wilaya ya Kinondoni ili kupata taarifa zaidi na kuona hatua zinazofaa.
Aidha, Dkt. Homera amesema kupitia Programu ya Sema na Waziri, Wizara imepokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wananchi, ambapo changamoto 19 zimekwishapatiwa ufumbuzi huku nyingine zaidi ya 30 zikiwa zimepokelewa na zikiendelea kufanyiwa kazi.
Amesema baadhi ya changamoto hizo zinahitaji ushauri wa kisheria, nyingine zinaelekezwa mahakamani, huku Wizara ikiendelea kufanya ufuatiliaji wa kina kwa zile zinazohitaji ushirikishwaji wa taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi.
Kuhusu upatikanaji wa haki kwa wafungwa na mahabusu, Dkt. Homera amesema Wizara itaendelea kufuatilia changamoto zao katika magereza mbalimbali nchini, akitoa mfano wa ziara ya hivi karibuni katika Gereza la Mahabusu Songea mkoani Ruvuma, ambapo wataalamu wa Wizara walifuatilia malalamiko ya kisheria yaliyowasilishwa na wafungwa na mahabusu.
Amesema lengo la hatua hizo ni kuhakikisha wananchi wanapata unafuu katika masuala ya kisheria na kwamba Wizara itaendelea kutumia programu mbalimbali ikiwemo Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Sema na Waziri pamoja na M-Semia kuwafikia wananchi na kushughulikia changamoto zao.
Akizungumzia mchakato wa mabadiliko ya Katiba, Dkt. Homera amesema suala hilo lipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030 na kwamba Serikali inaendelea na taratibu za ndani kwa mujibu wa sheria, huku akieleza kuwa muda ukifika mamlaka husika itatoa tamko rasmi kuhusu hatua zitakazofuata.
Amesema wananchi wanapaswa kuwa na subira wakati taratibu hizo zikiendelea, akisisitiza kuwa mabadiliko ya Katiba yanahitaji kufuata utaratibu wa kisheria ikiwemo kutungwa kwa sheria itakayoongoza mchakato huo.

