Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

MENEJA wa TARURA Wilaya ya Kilosa, Mhandisi Juliana Masaro, amesema wilaya hiyo imeanza kuchukua hatua za maandalizi kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua, ikiwemo kukagua , makaravati na mifereji ymadarajaa maji katika maeneo mbalimbali.

Mhandisi Masaro amesema Kilosa ni miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Morogoro zinazopokea maji mengi kutoka maeneo mbalimbali, hali inayofanya eneo hilo kuwa kama bakuli la maji na kusababisha mito mingi kupita katika maeneo yake.

Amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha changamoto kwa miundombinu ya barabara, licha ya TARURA kujitahidi kujenga madaraja makubwa katika maeneo yanayokumbwa na changamoto za maji.

“Ni kweli barabara zetu zinapata madhara sana kutokana na haya maji, lakini kwa kipindi hiki tumeshaanza kukagua madaraja yetu na mifereji yetu na kutoa taarifa kuhusu hatua tutakazochukua wakati mvua zitakapokuja,” amesema.

Mhandisi Masaro amesema TARURA tayari ina wakandarasi wanaotekeleza kazi kwa mwaka wa fedha 2026/27, hivyo dharura zitakapotokea, hatua zitachukuliwa kwa wakati kulingana na hali itakayojitokeza katika maeneo husika.

Amesema sambamba na wakandarasi hao, TARURA Wilaya ya Kilosa imeanza kutumia vikundi vya Community Based Routine Maintenance (CBRM), ambapo vikundi 17 vimeanza kazi katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya kusafisha na kuzibua makaravati, mifereji pamoja na kufanya matengenezo madogo ya barabara.

Amesema vikundi hivyo pia vimepewa mafunzo yatakayoviwezesha kuwafikishia wananchi elimu ya namna ya kujikinga na athari za mvua, ikiwemo kutoa taarifa kuhusu miti inayoanguka, maporomoko ya udongo na changamoto nyingine zinazoweza kuathiri barabara.

Kwa upande wake, Mratibu wa CBRM kutoka TARURA Makao Makuu, Richard Missa, amesema mpango huo unalenga kuboresha matengenezo ya barabara nchini kwa kuwashirikisha wananchi kupitia vikundi vya kijamii.

Missa amesema CBRM inatekelezwa chini ya Mradi wa Resilient Economic Opportunities and Roads, unaotumia fedha za Serikali pamoja na fedha kutoka Benki ya Dunia, huku mpango huo ukiwa na muda wa utekelezaji wa miaka mitatu.

Amesema miongoni mwa kazi zinazotekelezwa na vikundi hivyo ni kuzibua mifereji na makaravati, kusafisha madaraja, kufyeka nyasi kandokando ya barabara, kuondoa magogo na miti iliyoanguka pamoja na kurekebisha au kuweka alama za barabarani zilizoanguka.

Missa amesema mpango huo pia unalenga kuongeza ajira na kipato kwa wananchi wanaoishi karibu na barabara, ambapo vikundi hupewa mikataba ya kufanya matengenezo ya kawaida ya barabara huku vikiendelea na shughuli nyingine za kiuchumi.

Amesema mpango huo umeanza kutekelezwa katika mikoa mbalimbali, ambapo hadi sasa zaidi ya kilomita 1,500 zimeanza kufanyiwa matengenezo na vikundi 32 katika mikoa ya Tanga, Morogoro na Dodoma.

Missa amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27 mpango huo unatarajiwa kupanuka hadi zaidi ya kilomita 7,200 katika mikoa 25 na wilaya zaidi ya 140 nchini.

Amesema TARURA ipo katika hatua za mwisho za mchakato wa manunuzi kwa ajili ya kutoa mikataba kwa zaidi ya vikundi 1,400, ambapo kila kikundi kinatarajiwa kuwa na wanachama kati ya watano na 20.

Amesema ushiriki wa vikundi hivyo katika matengenezo ya kawaida ya barabara utasaidia kupunguza uharibifu unaoweza kusababishwa na maji ya mvua, kwa kuhakikisha mifereji, makaravati na maeneo ya kupitisha maji yanakuwa wazi na kufanya kazi kwa ufanisi.