Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa miundombinu katika Uwanja wa Ndege wa Msalato mkoani Dodoma unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 27, 2026, huku ujenzi wa majengo ukitarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 30, 2026.

Mhandisi Besta ameyasema  septemba 24,2026  akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukagua hatua za utekelezaji wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, ambapo amesema TANROADS inaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa programu za kazi ili kuhakikisha shughuli zote zinafanyika kwa mujibu wa ratiba iliyowekwa.

Amesema Wakala inaendelea kusimamia kwa karibu upatikanaji na ufungaji wa vifaa, pamoja na uratibu wa wakandarasi wanaotekeleza kazi mbalimbali katika mradi huo, ili kuhakikisha kazi zinazohusiana na kutegemeana zinatekelezwa kwa wakati na bila kuathiri ratiba ya mradi.

Aidha, Mhandisi Besta amesema TANROADS inaendelea kufuatilia utekelezaji wa kazi zinazotegemeana, huku taratibu mbalimbali za kimkataba zikikamilishwa kwa wakati. Amesisitiza kuwa hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha mradi unaendelea kwa ufanisi kuelekea tarehe zilizowekwa za kukamilisha ujenzi.

Amesema TANROADS itaendelea kufuatilia kwa karibu maendeleo ya mradi huo, kwa kushirikiana na wadau na wakandarasi wanaohusika, ili kuhakikisha kazi zilizobaki zinakamilishwa kwa wakati na Uwanja wa Ndege wa Msalato unafikia hatua iliyokusudiwa kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya kiuchumi ya Dodoma na Tanzania kwa ujumla.