Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mohamed Besta, amewataka Watanzania, hususani wakazi wa Dodoma, kutumia fursa zinazotokana na uwepo wa uwanja wa ndege wa Msalato katika kukuza uchumi wao binafsi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Mhandisi Besta amesema uwepo wa uwanja huo unatoa fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo biashara zinazohitaji usafirishaji wa haraka wa bidhaa kutoka sehemu moja kwenda nyingine. Amesema fursa hizo zinaweza kutumiwa na wafanyabiashara, wakulima na wadau wengine kuongeza thamani na kufikisha bidhaa zao kwenye masoko kwa wakati.

Ameeleza kuwa miongoni mwa bidhaa zinazoweza kunufaika na usafirishaji wa haraka kupitia uwanja huo ni mazao ya kilimo kama matunda na mboga mboga, samaki, kuku, maua pamoja na bidhaa nyingine zinazohitaji kufikishwa sokoni kwa muda mfupi ili kuhifadhi ubora na thamani yake.Aidha, Mhandisi Besta amesema uwanja huo una nafasi muhimu katika kukuza sekta ya utalii, kwa kurahisisha usafiri wa wageni kutoka ndani na nje ya Tanzania kuelekea Dodoma na maeneo mengine yenye vivutio vya utalii. Amesema fursa hiyo inapaswa kuangaliwa kwa mtazamo mpana zaidi kwa kuhusisha hoteli, usafirishaji, huduma za utalii na biashara ndogo na za kati.

Mhandisi Besta ametoa wito kwa Watanzania kutumia kikamilifu fursa hizo kwa kuanzisha na kuendeleza shughuli za kiuchumi zinazoweza kunufaika na huduma za usafiri wa anga, akisisitiza kuwa matumizi bora ya miundombinu iliyopo yanaweza kuchochea ajira, biashara na mapato, hivyo kuleta manufaa kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.