Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam
MATUMIZI ya mifumo ya kielektroniki katika malipo ya huduma za usafiri yameanza kupewa msukumo zaidi, huku maeneo mbalimbali ya sekta hiyo yakitakiwa kuzingatia utaratibu huo uliowekwa na Serikali.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), CPA Dkt. Habib Suluo, amesema utaratibu huo unalenga kurahisisha miamala na kuongeza uwazi katika huduma zinazohusisha usafiri na sekta nyingine za kiuchumi.
Akizungumza leo, Septemba 24,2026 24, 2026, jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya LATRA na wahariri wa vyombo vya habari nchini, Dkt. Suluo amesema matumizi ya njia za kielektroniki yanazingatia amri ya Waziri wa Fedha iliyotolewa kwa mujibu wa Kifungu cha 13(C) cha Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, Sura ya 442.
Amesema utaratibu huo ulianza kutumika rasmi Julai 1, 2026 na unahusisha maeneo mbalimbali ya huduma za usafiri, ikiwemo malipo ya ada, tozo na ushuru unaohusiana na sekta hiyo.¹
Aidha CPA Dkt. Suluo, amesema matumizi ya malipo ya kielektroniki yanahusisha pia nauli za mabasi ya mijini, mabasi yaendayo haraka (BRT), vivuko na madaraja, hivyo kubadili namna wananchi wanavyofanya miamala katika huduma hizo.
Amesema mabasi yanayotoa huduma za masafa marefu kati ya mikoa nayo yanapaswa kutumia mifumo ya kielektroniki katika kupokea nauli, badala ya kutegemea fedha taslimu pekee.
Aidha, amesema utaratibu huo unahusu huduma za teksi mtandao, usafiri wa reli na malipo ya maegesho ya magari, huku LATRA ikiendelea kutoa elimu kwa wasafirishaji na wananchi kuhusu utekelezaji wa matakwa hayo.
Dkt. Suluo amesema hata katika matumizi ya magari, wamiliki na waendeshaji wanapaswa kutumia njia za kielektroniki wanapofanya malipo ya mafuta katika vituo vya huduma, akieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mfumo mpana wa miamala ya kielektroniki.
Ameongeza kuwa baadhi ya huduma za hoteli, migahawa na utalii, pamoja na miamala ya ununuzi na uuzaji wa magari, pia zimejumuishwa katika utaratibu huo, unaolenga kuongeza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
