Makatibu Wakuu wanaosimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), na sekta ya biashara kutoka Nchi Wanachama wamekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wa hatua za kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara ndani ya Jumuiya.
Makubaliano hayo yamefikiwa leo, Septemba 24, 2026, katika Mkutano wa Kikanda wa Makatibu Wakuu unaofanyika jijini Dar es Salaam, unaolenga kupitia utekelezaji maelekezo ya Mkutano wa 25 wa Wakuu wa Nchi za EAC, uliofanyika Arusha tarehe 7 Machi 2026, ambao ulizitaka Nchi Wanachama kushughulikia na kuondoa vikwazo vyote vya biashara visivyo vya kodi vilivyoripotiwa ndani ya Jumuiya ifikapo Juni 30, 2026.
Vilevile, mkutano huo umejikita katika kutathmini hali ya utekelezaji na kuweka hatua za haraka za kushughulikia Vikwazo Visivyo vya Kodi (Non-Tariff Barriers – NTBs) vinavyoendelea kuathiri biashara miongoni mwa Nchi Wanachama.
Mbali na hilo, Makatibu Wakuu wamekubaliana kuharakisha utekelezaji wa hatua za kuondoa ushuru, ada, tozo na kodi za ndani zinazobagua bidhaa zinazotoka katika Nchi Wanachama, kwa kuzingatia matakwa ya Ibara ya 10 na 15 ya Itifaki ya Umoja wa Forodha ya EAC.
Hatua hiyo inalenga kuweka mazingira sawa ya ushindani kwa bidhaa zinazozalishwa na kuuzwa ndani ya Jumuiya, kupunguza gharama za kufanya biashara na kurahisisha mtiririko wa bidhaa katika mipaka ndani ya Jumuiya.
Akizungumza katika mkutano huo, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayesimamia Masuala ya Afrika Mashariki, Bw. Charles Ngeleja Kadonya, amesema Tanzania itaendelea kutekeleza mipango, maamuzi na makubaliano yanayofikiwa na Nchi Wanachama kwa lengo la kuimarisha mtangamano wa kikanda na kuongeza manufaa kwa wananchi.
Amesisitiza umuhimu wa Nchi Wanachama kuhakikisha maamuzi yanayofikiwa katika ngazi ya Jumuiya yanatekelezwa kwa wakati, ili kuondoa vikwazo vinavyoongeza gharama na kuchelewesha biashara, pamoja na kuimarisha ufanisi wa mifumo ya biashara na usafirishaji katika ukanda huo, ikiwemo Vituo vya Huduma Pamoja Mpakani (OSBP’s).
Mkutano huo unafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 22 hadi 25, 2026, ukihusisha ngazi ya Wataalamu na Makatibu Wakuu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za EAC kuimarisha utekelezaji wa makubaliano ya kikanda, kuondoa vikwazo vya biashara na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa, huduma na mitaji ndani ya Jumuiya.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umeongozwa na Katibu Mkuu Bw. Charles Ngeleja Kadonya, akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar Dkt. Habiba Hassan Omar, pamoja na watendaji waandamizi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali.

