Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MANISPAA ya Kibaha imeendelea kusimamia utekelezaji wa maagizo ya utunzaji wa mazingira kwa viwanda, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na madhara yanayoweza kujitokeza wakati wa mvua za El Niño zinazotarajiwa.
Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda kuboresha mifumo ya kuchuja na kutiririsha maji taka, ili kuzuia maji hayo kusambaa katika maeneo ya wananchi na kusababisha madhara kwa jamii na mazingira.
Dkt. Mawazo ametoa wito huo wakati akikagua kiwanda cha kutengeneza karatasi cha Fortune, kilichopo Misugusugu, ikiwa ni sehemu ya ziara ya kufuatilia utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Manispaa kuhusu utunzaji wa mazingira.
Amesema kiwanda hicho awali kilikuwa na mashimo manne makubwa yaliyotumika kutiririsha maji taka, hali iliyokuwa ikihatarisha wananchi wanaoishi maeneo ya jirani, lakini katika ukaguzi huo amebaini kuwa maagizo ya Manispaa yametekelezwa kwa mashimo hayo kufukiwa na mfumo wa majitaka kuboreshwa.
Meya Mawazo amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wawekezaji kwa kuwa viwanda vinachangia pato la Serikali na kutoa ajira, huku akiwataka kuzingatia sheria na miongozo ya utunzaji wa mazingira.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Saeni, Edward Kitale, amesema wananchi walikuwa wakikabiliwa na kero ya harufu mbaya pamoja na maji taka kuelekea mashambani, lakini hali hiyo imeanza kuimarika baada ya mashimo hayo kufukiwa.
Naye Ofisa Mazingira wa kiwanda hicho, Daudi Tito, amesema wamepokea maelekezo ya Serikali na Manispaa na wataendelea kuzingatia sheria na miongozo ya mazingira ili changamoto hiyo isijitokeze tena.
Meneja Biashara wa kiwanda hicho, Colin Tang, amesema kiwanda kimeboresha mifumo yake kwa kujenga mitambo ya kisasa ya kuchuja maji taka, hatua inayolenga kuzuia madhara kwa wananchi na mazingira.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi, Meya Dkt. Mawazo pia amekagua kiwanda cha kutengeneza mabati na bidhaa za chuma cha Kinglion, pamoja na Shule ya Sekondari na Shule ya Msingi Misugusugu.

