Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akipokea tuzo kutoka kwa Dkt. Mwatima Juma, Mwenyekiti wa Bodi ya PPIZ, wakati wa uzinduzi wa Tamasha la Kilimo Hai Dole Kizimbani, Zanzibar, leo 23 Septemba 2026.

………… 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema kilimo ni miongoni mwa sekta za msingi katika uchumi wa Zanzibar, hivyo Serikali itaendelea kuwekeza katika kuimarisha miundombinu ya uzalishaji, matumizi ya teknolojia za kisasa, mifumo ya umwagiliaji, upatikanaji wa mikopo nafuu pamoja na masoko ya mazao ya kilimo.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 23 Septemba 2026, wakati akifungua Tamasha la Tatu la Kilimo Hai Zanzibar (Zanzibar Organic Festival) la mwaka 2026, Dole Kizimbani, Wilaya ya Magharibi “A”, Unguja.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inalenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa chakula kwa gharama nafuu, huku wakihifadhi rutuba ya udongo na vyanzo vya maji pamoja na kuhakikisha usalama wa chakula na afya za walaji.

Amesisitiza kuwa kilimo hai na kilimo ikolojia (kilimo kinachozingatia afya ya udongo, maji na mazingira) vinapaswa kuwa sehemu muhimu ya mustakabali wa maendeleo ya Zanzibar kutokana na mchango wake katika uzalishaji endelevu wa chakula, afya ya jamii na utunzaji wa mazingira.

Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali imezindua Mkakati wa Kilimo Hai wa Zanzibar, ambao utekelezaji wake utahusisha maeneo mbalimbali yakiwemo uzalishaji wa shambani, bajeti, huduma za ugani, upatikanaji wa pembejeo, tafiti pamoja na kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa mazao ya kilimo.

Ameeleza kuwa kilimo hai si suala la uzalishaji wa chakula pekee, bali kinahusisha pia afya ya mazingira, ustawi wa wananchi na uwezo wa Zanzibar kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi ameiagiza Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo kuanza mchakato wa kuanzisha Kitengo Maalum cha Kilimo Hai kitakachoratibu shughuli zote zinazohusiana na kilimo hai Zanzibar.

Aidha, ameielekeza Wizara hiyo kufanya tathmini ya uwezekano wa kujumuisha pembejeo za kilimo hai katika mpango wa ruzuku ya pembejeo za kilimo, ili kuongeza upatikanaji wake kwa wakulima.

Rais Dkt. Mwinyi pia amesisitiza umuhimu wa matumizi salama na sahihi ya pembejeo za kilimo, akieleza kuwa Serikali itaendelea kudhibiti pembejeo hatarishi, kufuatilia matumizi yake na kutoa elimu kwa wakulima ili kuhifadhi mazingira na kuhakikisha usalama wa mazao na afya za walaji.

Akizungumzia uhusiano kati ya kilimo na utalii, Rais Dkt. Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji kuimarisha mfumo wa “Shambani hadi Mezani” (Farm-to-Table), kwa kuongeza matumizi ya mazao yanayozalishwa na wakulima wa Zanzibar katika hoteli na mikahawa.

Amesema mfumo huo utawapatia wakulima masoko yenye uhakika na thamani zaidi, kuongeza kipato chao na wakati huo huo kuiwezesha sekta ya utalii kupata chakula bora na salama kinachozalishwa Zanzibar.

Rais Dkt. Mwinyi amezihimiza hoteli, mikahawa na wasambazaji wa chakula kuongeza ununuzi wa mazao kutoka kwa wakulima wa Zanzibar, huku Serikali ikiendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayowawezesha wakulima kuongeza uzalishaji na kufikia masoko yenye thamani.

Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Kilimo Hai Zanzibar (Zanzibar Organic), Ndugu Ikram Ramadhan Soraga, amesema tamasha hilo linalenga kuwakutanisha wakulima na wadau mbalimbali, kuwaunganisha na fursa za biashara na masoko pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kilimo hai.

Tamasha la Tatu la Kilimo Hai limebeba kaulimbiu “Fikiri Kiulimwengu, Kula Kiasili”, likiwa jukwaa la kubadilishana uzoefu, maarifa, teknolojia na ubunifu katika sekta ya kilimo, pamoja na kuhamasisha matumizi ya mbinu bora na endelevu za uzalishaji wa chakula.

Katika Tamasha hilo, Rais Dkt. Mwinyi ametoa tuzo kwa wadhamini na wadau mbalimbali wanaounga mkono juhudi za Serikali katika kuendeleza sekta ya kilimo.

Rais Dkt. Mwinyi pia ametunukiwa tuzo ya heshima kwa kutambua uongozi na mchango wake katika juhudi za kuendeleza sekta ya kilimo Zanzibar.