MBUNGE wa Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, Jackson .Kiswaga, leo ameshiriki Mkutano wa 9 wa Kimataifa kuhusu Milango ya Mito na Maeneo ya Pwani (International Conference on Estuaries and Coasts), unaofanyika katika mji wa Qinzhou, Mkoa wa Guangxi nchini China.
Mkutano huo unaofanyika kuanzia Septemba 22 hadi 26, 2026, umewakutanisha watafiti, wataalamu wa ikolojia na wadau kutoka mataifa mbalimbali duniani kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na maarifa kuhusu uhifadhi na usimamizi wa milango ya mito pamoja na maeneo ya pwani.
Mkutano huo unalenga kujadili changamoto zinazokabili milango ya mito na maeneo ya pwani, ikiwemo athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, mmomonyoko, mafuriko na matukio mengine ya kimazingira yanayoweza kubadilisha mifumo ya asili ya maeneo hayo.
Milango ya mito ni maeneo ambayo maji ya mito yanapokutana na bahari, hivyo kuwa na umuhimu mkubwa katika mfumo wa ikolojia, mazingira, uchumi na maisha ya jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Kutokana na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa, ikiwemo mafuriko na vimbunga, baadhi ya maeneo ya milango ya mito yamekuwa yakibadilika kijiografia na kimazingira, hali inayohitaji tafiti za kisayansi na hatua za kiikolojia ili kuelewa mabadiliko hayo na kutafuta njia sahihi za kuyadhibiti.
Ushiriki wa Kiswaga katika mkutano huo unakuja wakati ambapo Tanzania ikiendelea kuhitaji mijadala na ushirikiano wa kimataifa katika kulinda rasilimali za maji na mazingira.
Kiswaga pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, na hivi karibuni amekuwa miongoni mwa viongozi wa Tanzania waliokutana na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, ambapo walijadili namna ya kupanua ushirikiano katika sekta za maji na uhifadhi wa mazingira.
Mkutano wa Qinzhou umeandaliwa chini ya usimamizi wa China Institute of Water Resources and Hydropower Research (IWHR), kwa kushirikiana na Serikali ya Mji wa Qinzhou pamoja na taasisi nyingine zinazohusika na maji, usafirishaji, mmomonyoko na uhifadhi wa maeneo ya pwani.
Mjadala wa kimataifa unaendelea kusisitiza umuhimu wa kutumia tafiti na teknolojia za kisasa katika kufuatilia mabadiliko ya milango ya mito na maeneo ya pwani, huku nchi zikishirikiana kutafuta mbinu zinazoweza kusaidia kulinda mazingira na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.
