Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Maswi, amesema wazee si wapokeaji wa huduma pekee bali ni hazina ya maarifa, uzoefu, historia, maadili, busara na utaalamu unaopaswa kutumika katika kujenga taifa.

Ameyasema hayo Septemba 23, 2026 jijini Dodoma wakati akizungumza katika kikao na uongozi wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, akibainisha kuwa wazee pia ni walezi wa familia, wasuluhishi wa migogoro, walimu wa maisha na walinzi wa mshikamano wa jamii.

Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 unapaswa kutambua mahitaji ya wazee na kutumia kikamilifu uwezo, busara na uzoefu wao katika kujenga taifa, kwa kuwa Dira hiyo inalenga taifa lenye ustawi, usawa, haki na maendeleo jumuishi.

Aidha, amebainisha kuwa Wizara inaendeleza Jamii Agenda 2050 yenye msingi wa falsafa ya Familia Imara, Jamii Imara, Taifa Imara, akisisitiza kuwa taifa imara haliwezi kujengwa kwa kuwaacha wazee pembeni.

Pia ameongeza kuwa idadi ya wazee nchini imeongezeka kutoka milioni 2.5 mwaka 2012 hadi milioni 3.4 mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 35.8, huku wastani wa umri wa kuishi ukiongezeka kutoka miaka 61.7 hadi miaka 67.2.

Amesema ongezeko hilo linaweka wajibu wa kujiandaa zaidi katika maeneo ya afya, bima na hifadhi ya jamii, makazi, lishe, huduma za matunzo, usalama, ushiriki wa wazee katika shughuli za kiuchumi na ulinzi dhidi ya ukatili na unyanyasaji wa mali.

Amesema hadi Juni 2026 jumla ya mabaraza ya wazee 20,768 yalikuwa yameundwa nchini, akisisitiza kuwa mafanikio yake hayatapimwa kwa idadi ya mabaraza pekee, bali kwa namna yanavyoboresha maisha ya wazee.

Aidha, ameyataka mabaraza hayo kuwa na nguvu ya kuishauri Serikali, kufuatilia utekelezaji wa haki, sera na miongozo inayohusu wazee, kubaini changamoto na fursa zao na kuhakikisha masuala yao yanaingizwa katika mipango na bajeti.

Pia, amebainisha kuwa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa linapaswa kuwa daraja kati ya wazee, jamii, Serikali na wadau wengine, huku likitoa taarifa kuhusu ukatili, unyanyasaji, mauaji na unyang’anyi wa mali za wazee.

Pia ameongeza Kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha ushirikiano na Baraza hilo, akisisitiza kuwa mabaraza ya wazee hayapaswi kuwa ya jina tu au kwa ajili ya mikutano na sherehe pekee, bali yawe vyombo vyenye nguvu katika ushauri, uwakilishi, ufuatiliaji na uwajibikaji kuhusu masuala ya wazee.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa, David Sendo, amesema maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yatafanyika Oktoba 1, 2026 katika ngazi za mikoa, wilaya, halmashauri, kata na vijiji, huku kilele cha kitaifa kikifanyika Novemba 5, 2026 mkoani Songwe, na Novemba 4 kutakuwa na kongamano la Baraza la Wazee.

Amebainisha Kuwa kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee Taifa cha Oktoba 1 na 2, 2026 kitajadili uendeshaji wa mabaraza ya wazee, bajeti, upatikanaji wa ofisi, uhai wa mabaraza, makazi ya wazee na maandalizi ya maadhimisho ya kitaifa, huku akisema kaulimbiu ya mwaka huu ni “Zama za maisha marefu, tuboreshe huduma kwa wazee.”