Na Hellen Mtereko,Mwanza

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewaonya madereva wanaoendesha pikipiki za mizigo aina ya Guta baada ya kubainika kuwa baadhi yao wamekuwa wakipakia mizigo kwa namna inayohatarisha usalama wao na watumiaji wengine wa barabara.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya kutoa elimu kwa madereva hao, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amesema Jeshi la Polisi limekuwa likipokea taarifa kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya madereva wa pikipiki za magurudumu matatu wanaokiuka sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani, hususan katika upakiaji wa mizigo.

Amesema taarifa hizo zilifanyiwa kazi na Jeshi la Polisi kujiridhisha kuwa vitendo hivyo vinaendelea, ambapo katika hatua hiyo madereva 72 pamoja na vyombo vyao na mizigo walikamatwa na kupewa elimu.

Kamanda Mutafungwa amesema upakiaji huo ni hatari kwa kuwa vyombo hivyo hutumia barabara zinazotumiwa na makundi mbalimbali ya wananchi, wakiwemo watembea kwa miguu, wanafunzi na madereva wa magari, hivyo kitendo cha kubeba mizigo inayozidi ukubwa wa chombo kinaweza kusababisha ajali na madhara makubwa.

Amesema tayari kumekuwa na matukio ya ajali yanayohusishwa na upakiaji wa mizigo kwa namna hatarishi, akitoa mfano wa chombo cha magurudumu matatu kilichokuwa kimebeba miringoti iliyotoka nje ya upana wa chombo na kugonga gari lililokuwa likitokea mbele, hali iliyosababisha dereva kupoteza maisha.

Kamanda Mutafungwa amewataka madereva hao kutambua kuwa barabara ni ya watumiaji wote na kwamba wanapaswa kuzingatia usalama wa wengine wakati wanapofanya shughuli zao za usafirishaji.

Aidha, amesema Jeshi la Polisi limeamua kutoa elimu kwa madereva hao badala ya kuchukua hatua za kisheria pekee, huku akimuelekeza mkuu wa Kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Mwanza Ssp Sunday Ibrahim kuandaa kikao cha elimu kwa madereva hao kufanyika siku ya Ijumaa ili kuwasaidia kuelewa madhara ya ukiukwaji wa sheria na taratibu za usalama barabarani.

Kamanda Mutafungwa amewataka madereva kuwa makini wanapokuwa barabarani kwa kuhakikisha wanatazama pande zote na kutoa nafasi kwa watumiaji wengine wa barabara kabla ya kuendelea na safari.

“Watumiaji wa barabara si wao pekee, kila mmoja ana haki ya kutumia barabara, hivyo ni muhimu kuzingatia usalama wa wengine kwa kutazama kushoto na kulia kabla ya kukata kona au kuingia kwenye barabara nyingine,” amesema.