Zaidi ya Kaya 40 katika Kijiji cha Marieni, Kata ya Chome, Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro, zimeagizwa kuhama baada ya ardhi kusogea na kusababisha nyufa kubwa, hali ambayo tayari imeharibu takribani nyumba 10 pamoja na kanisa moja.
Serikali imesema hatua hiyo ni ya haraka kutokana na hatari ya kutokea kwa maafa katika eneo hilo lenye milima na miteremko, huku kukiwa na uwezekano wa miamba kuporomoka.
Agizo hilo limetolewa baada ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), chini ya Wizara ya Madini, kufanya utafiti na kubaini mabadiliko ya kijiolojia yanayoendelea chini ya ardhi.
Mjiolojia Mwandamizi wa GST, Gabriel Mbogoni, amesema utafiti umebaini uwepo wa tabaka nene la udongo wa mfinyanzi lenye maji, hali inayosababisha ardhi kupoteza uimara na kuongeza uwezekano wa kusogea au kuporomoka.
Kwa mujibu wa Mbogoni, nyufa zimeonekana kuanzia maeneo ya juu ya mlima hadi mashambani na karibu na kanisa lililoharibiwa. Ameongeza kuwa baadhi ya miundombinu ya zege imeonekana kuinuka kutokana na msukumo unaotokea chini ya ardhi.
Amesema vipimo vya jiolojia na usumaku vimeonesha pia uwepo wa maeneo yenye tabaka kubwa la udongo wa mfinyanzi. Hata hivyo, amesema hali hiyo imetokana na mchakato mrefu wa kijiolojia, huku shughuli za binadamu zikichangia kudhoofisha zaidi ardhi hiyo.
Miongoni mwa shughuli hizo ni ukataji wa miti, kilimo na matumizi ya mifereji ya wazi ya umwagiliaji, ambayo husababisha maji kubaki ardhini kwa muda mrefu na kupunguza uimara wa udongo wa mfinyanzi.
Mkuu wa Wilaya ya Same, Rukia Zuberi, amesema baada ya kupokea maelezo ya wataalamu, Serikali imebaini kuwa maeneo hayo si salama tena kwa makazi wala shughuli za maendeleo.
Amesema wananchi wanapaswa kuondoka haraka, huku akiwaagiza viongozi wa Halmashauri, kata na vijiji kuanza mchakato wa kutafuta maeneo salama kwa ajili ya makazi ya kudumu.
Pia amewataka wananchi kuchukua hatua mapema kuokoa maisha na mali zao badala ya kusubiri maafa yatokee.
Rukia amesema maporomoko ya ardhi yanaweza kutokea wakati wowote na muda wake hauwezi kutabirika kwa usahihi. Amesisitiza kuwa tahadhari hiyo haiwahusu wakazi wa Chome pekee, bali wote wanaoishi katika maeneo yaliyobainishwa kuwa hatarishi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Makandeni, Marry Abuduel, amesema wamepokea maelekezo ya Serikali na wako tayari kuyatekeleza, lakini changamoto kubwa ni upatikanaji wa maeneo salama ya kuwapeleka watakaohama.
Abuduel ameomba TANESCO kuchukua hatua kuhusu baadhi ya nguzo za umeme zilizopo katika eneo hilo, akisema zimekuwa zikitumika kwa zaidi ya miaka 26, huku nyingine zikianza kuoza na baadhi ya nyaya kuwa karibu na maeneo yenye nyufa.
Kwa upande wake, mwananchi Elisa Mtera amesema hali hiyo imewaweka wananchi katika hofu kubwa kutokana na kuendelea kwa nyufa, huku familia zikikabiliwa na changamoto ya kukosa maeneo ya kwenda endapo wataondoka.
Amesema wananchi, wazazi na watoto hawaishi kwa amani kutokana na hofu ya kutokea kwa maafa, hasa wakati wa msimu wa mvua, na kuiomba Serikali kuwapatia maeneo mbadala kwa haraka.

