Shirika la Foundation for Disabilities Hope (FDH) limeipongeza Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Tanzania (PSPTB) kwa juhudi zake za kuhakikisha watu wenye ulemavu wanajumuishwa katika utoaji wa huduma na shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mtendaji wa FDH, Maiko Salali, amesema shirika hilo limeamua kutumia jukwaa hilo kutambua na kupongeza taasisi za Serikali na zisizo za Serikali ambazo zimekuwa zikitoa mchango katika kuwawezesha watu wenye ulemavu.
Amesema FDH inatambua mchango wa PSPTB katika kujenga mazingira rafiki na wezeshi kwa watu wenye ulemavu, ikiwemo kuhakikisha wanapata fursa ya kushiriki katika masuala ya ununuzi, ugavi na utoaji wa huduma.
“Tunatumia fursa hii kupongeza sana Bodi ya PSPTB kwa mchango mkubwa ambao imekuwa ikifanya katika kuwawezesha watu wenye ulemavu na kuhakikisha wanajumuishwa katika utoaji wa huduma,” amesema Salali.
Amesema juhudi hizo ni sehemu muhimu ya kujenga jamii jumuishi ambayo haimuachi mtu yeyote nyuma, hususan katika upatikanaji wa huduma, miundombinu rafiki na fursa mbalimbali.
Salali ameongeza kuwa FDH inathamini namna uongozi wa PSPTB, ukiongozwa na mkurugenzi mtendaji, CPSP. Godfred Mbanyi, unavyozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Aidha, ameupongeza uongozi na menejimenti ya PSPTB kwa kuendelea kutekeleza kwa vitendo misingi ya ujumuishaji wa watu wenye ulemavu.
Katika hatua nyingine, Salali amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema uongozi wake umeendelea kutoa msukumo katika kuhakikisha makundi mbalimbali, wakiwemo watu wenye ulemavu, yanazingatiwa katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.
Amesema taasisi za Serikali zinapaswa kuendelea kutafsiri kwa vitendo maono ya Serikali kuhusu ujumuishaji na ushirikishwaji wa watu wenye ulemavu.
“Tunajivunia kuona jitihada zinazolenga kujenga jamii inayozingatia mahitaji ya watu wote, ikiwemo watu wenye ulemavu,” amesema.
Salali amezitaka taasisi nyingine za umma na binafsi pamoja na bodi mbalimbali kujifunza kutokana na juhudi zinazofanywa na PSPTB katika kuwawezesha na kuwajumuisha watu wenye ulemavu.
Amesema ushirikishwaji huo ni muhimu katika kujenga jamii yenye usawa, inayotoa fursa kwa kila mtu kushiriki katika shughuli za kijamii na kiuchumi bila ubaguzi.
FDH imeendelea kutoa wito kwa taasisi zote nchini kuweka mazingira rafiki na jumuishi kwa watu wenye ulemavu ili kuhakikisha hakuna kundi linaloachwa nyuma.
