Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, akiagana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya CAM SARL, Bouzid Belhad, ambayo hutengeneza mashine za kusindika na kufungasha dawa na mazao ya kilimo. Kushoto ni Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa CAM, Abderraouf Belhadj, na kulia ni Mkurugenzi wa Uendeshaji, Alaaeddine Belhadj.
……………..
Na Mwandishi Wetu
Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mhe. Mobhare Matinyi, leo Septemba 23, 2026, alifanya ziara katika kiwanda cha kampuni ya CAM SARL kilichoko nje kidogo ya jiji la Algiers, kinachotengeneza mashine za kusindika na kufungasha mazao ya kilimo na dawa za tiba.
Katika ziara hiyo, Balozi Matinyi alifanya majadiliano na timu ya menejimenti ya kampuni hiyo iliyoongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu Bouzid Belhadj, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha Abderraouf Belhadj, na Mkurugenzi wa Uendeshaji Alaaeddine Belhadj.
Lengo la majadiliano hayo lilikuwa kuangalia uwezekano wa kampuni hiyo kutengeneza mashine mahsusi kwa ajili ya kusindika na kufungasha mazao yanayolimwa nchini.
Balozi Matinyi aliielezea kampuni ya CAM kwamba Serikali ya Tanzania imeweka sera na mikakati ya kuhakikisha bidhaa za kilimo za Tanzania zinaongezewa thamani kabla ya kuuzwa kwenye soko la kimataifa.
Akitoa mifano ya mazao ya chakula yanayolimwa nchini, kama matunda, mbogamboga, viungo, nafaka, korosho, karanga na hata alizeti, chai na kahawa, Balozi Matinyi alielezea matumaini yake kwamba ushirikiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Algeria utaiwezesha kampuni hiyo kutoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo nchini.
Mtendaji Mkuu wa CAM, Belhadj, alimshukuru Balozi Matinyi kwa ziara hiyo na kuahidi kuendeleza ushirikiano na Tanzania pamoja na kufanya ziara nchini ili kujionea fursa na mahitaji yaliyopo.
Kampuni ya CAM hutumia wataalamu wa Algeria kutengeneza mashine hizo kwa kutumia teknolojia ya nchi za Ujerumani, Italia na Hispania, na tayari imeshaanza kuingia katika masoko ya nchi jirani na Algeria ikiwemo Tunisia.
