Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), (kulia), akiagana na Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Chotto Sendo, aliyemwakilisha Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El -Maamry Mwamba, katika Mkutano wa 19 wa Mwaka wa Ukaguzi wa Ndani pamoja na Jukwaa la 13 la Utawala Bora, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa ndani Tanzania (The Institute of Internal Auditors- Tanzania, kushoto ni Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi, Kenneth Nindie.
Na. Asia Singano, WF – Arusha.
Wizara ya Fedha, imeanza mchakato wa kuanzisha Sheria Maalum ya Ukaguzi wa Ndani ikiwa ni hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa udhibiti wa ndani na kuweka msingi imara wa kisheria na kitaasisi kwa shughuli za ukaguzi nchini.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), kupitia Hotuba yake iliyosomwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), alipomwakilisha katika Mkutano wa 19 wa Mwaka wa Ukaguzi wa Ndani pamoja na Jukwaa la 13 la Utawala Bora, uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), ulioandaliwa na Taasisi ya Ukaguzi wa Ndani Tanzania (The Institute of Internal Auditors- Tanzania).
Alisema hatua hiyo inalenga kuweka msingi imara wa kisheria na kitaasisi utakaowezesha kuboresha mfumo wa ukaguzi wa ndani, ikiwemo kuimarisha majukumu ya wadau mbalimbali wanaohusika na ukaguzi pamoja na kamati za ukaguzi.
‘’Sheria mahsusi ya Ukaguzi wa Ndani itasaidia kuweka wazi majukumu, mamlaka, mipaka ya kiutendaji na mahusiano ya kikazi kati ya Ukaguzi wa Ndani, Menejimenti na Kamati za Ukaguzi’’ alisema Mhe. Luswetula
Aliongeza kuwa, Wizara inaendelea na mchakato wa kuhuisha muundo wa kiutumishi wa Kada ya Ukaguzi wa Ndani (Scheme of Service), ili kutambua na kuruhusu ushiriki wa wataalamu wenye taaluma mbalimbali ikiwemo wahandisi, madaktari katika kazi za ukaguzi ili kuongeza wigo wa utaalamu katika Ukaguzi wa Ndani, kwa kuzingatia mahitaji na vihatarishi mahsusi vya sekta mbalimbali, tofauti na mfumo wa sasa unaozingatia zaidi taaluma za Uhasibu na Fedha.
Alibainisha kuwa maendeleo ya kitaaluma ya Wakaguzi wa Ndani ni jukumu la pamoja, linalohitaji ushirikiano wa Wizara ya Fedha, Wakuu wa Taasisi na Maafisa Masuuli wa Taasisi husika.
‘’Kwa msingi huo, natoa wito kwa Viongozi wa Taasisi kuendelea kuwajengea uwezo Wakaguzi wa Ndani na Kamati za Ukaguzi, ili kuimarisha ufanisi katika usimamizi wa rasilimali na kuongeza mchango wao katika kufanikisha malengo ya taasisi’’ alisema Mhe. Luswetula
Akizungumza kwa niaba ya Mhe. Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu- Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum (Mb), aliwataka wakaguzi wa ndani kufanya kazi kwa ufanisi na weledi ili kujenga uaminifu kwa wananchi.
‘’Wakaguzi wa ndani mnapaswa kuendelea kusaidia taasisi kuhakikisha kuwa rasilimali zinatumika kwa ufanisi tija na kwa kuzingatia thamani ya fedha, katika kila rasilimali inayotumika kwa ufanisi inaongeza uwezo wa taifa kuboresha huduma za afya elimu, kilimo, miundombinu na huduma nyingine muhimu kwa wananchi’’ alisema Mhe. Saada Mkuya
Alisema kuwa Serikali itaendelea kujizatiti katika kuimarisha utawala bora, kuboresha usimamizi wa fedha za umma na kuunga mkono jitihada zinazolenga kuongeza uwajibikaji katika sekta za umma na binafsi.
Kwa upande wake Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, aliwaagiza wakaguzi wa ndani kuendelea kutumia mifumo ya ukaguzi ili kuhakikisha usimamizi wa vihatarishi katika taasisi za umma unatumia mfumo ili kulinda fedha za umma.
‘’Niombe wakuu wa taasisi tuwatake Wakaguzi wetu wa Ndani watumiwe, lakini pia tuwawezeshe kutumia mifumo ya ukaguzi wa ndani’’ alisema Mhandisi Nindie.
Mkutano wa 19 wa Mwaka wa Ukaguzi wa Ndani wenye kauli mbiu zaidi ya uhakikiso: Kuendesha Ufahamu Ubunifu na Kuaminika’’ (Beyond Assurance: Driving insight, innovation and Trust), pamoja na Jukwaa la 13 la Utawala Bora, umewakutanisha wataalamu wa Ukaguzi wa Ndani, Viongozi wa Serikali, Bodi na Menejimenti, Mamlaka za Udhibiti, Sekta binafsi, Taasisi za Kitaaluma pamoja na wadau mbalimbali, kwa ajili ya kujadili kwa kina masuala ya Utawala bora, Uwajibikaji, Usimamizi wa Vihatarishi, Uadilifu na Ufanisi wa Taasisi.

