Mwamvua Mwinyi, Pwani
Septemba 22, 2026
WAKULIMA mkoani Pwani wametakiwa kuendelea kuandaa mashamba na kupanda mazao mbalimbali, ikiwemo yale yanayostahimili unyevu na mvua nyingi, huku wakizingatia ushauri wa wataalamu kufuatia utabiri wa mvua za msimu wa Vuli unaotarajiwa kuathiriwa na hali ya El Niño.
Kaimu Ofisa Hali ya Hewa mkoani Pwani ,Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mussa Nkucha alitoa ushauri huo kufuatia utabiri wa mvua za msimu wa Vuli, Oktoba hadi Desemba 2026, ambazo zinatarajiwa kuwa za juu ya wastani hadi wastani katika maeneo mbalimbali, zikiambatana na unyevu mwingi ardhini na uwezekano wa mafuriko.
Alitoa rai kwa wakulima kupanda kwa wakati, kwa kuzingatia tarehe za kuanza kwa mvua katika maeneo yao, ambazo zinatarajiwa kuanzia wiki ya nne ya Septemba hadi Oktoba.
Aidha, Mussa aliwashauri wakulima kuchimba mifereji ya kupitisha maji ya ziada na kuweka matuta kinga ili kudhibiti maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kulinda rutuba ya mashamba.
Kadhalika kutumia mbinu na teknolojia zinazosaidia kuzuia maji kutuama shambani, hali ambayo inaweza kusababisha mizizi ya mazao kuoza, pamoja na kuweka miundombinu ya kuvuna maji ya mvua ili maji ya ziada yaweze kutumika katika vipindi vya ukavu au msimu unaofuata.
“Wakulima wawasiliane kwa karibu na Maafisa Ugani katika maeneo yao ili kupata ushauri unaozingatia aina ya udongo, mazao na hali ya hewa ya maeneo yao.”
Pia aliwaasa wakulima na wananchi kufuatilia taarifa na utabiri wa hali ya hewa unaotolewa kila siku ili kuchukua hatua stahiki kulingana na mabadiliko ya hali ya hewa.

