New York, Marekani

Ikishiriki Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu ya Viongozi pembezoni mwa Mkutano wa 81 wa United Nations General Assembly (UNGA 81), Tanzania yaweka msisitizo juu ya msimamo wake wa kuhakikisha uongezaji thamani wa madini mkakati unafanyika ndani ya nchi yanamochimbwa kabla ya kusafirishwa kwenda nje.

Hayo yamesemwa leo tarehe 21 Septemba, 2026 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony P Mavunde alipomwakilisha 

Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Maalum wa Ngazi ya Juu wa Viongozi kuhusu maendeleo ya madini mkakati Barani Afrika.

Alisema baadhi ya Nchi za Afrika zinadhani msimamo wa kutaka madini mkakati kuongezwa thamani ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa nje unachelewesha uwekezaji.

“Niwaombe wenzangu katika Bara la Afrika tusilegeze masharti yetu kwa kisingizio cha kuvutia uwekezaji, kwani uongezaji thamani madini ndani ya Nchi ni nguzo muhimu ya kuendeleza Nchi zetu hususan katika kufikia manufaa tarajiwa kwenye uvunaji wa madini mkakati,” alisisitiza Waziri Mavunde.

Aidha, Waziri Mavunde alibainisha kuwa Nchi za Afrika zinapoweka msimamo wa kuongeza thamani madini mkakati ndani ya Nchi zinajiweka katika ramani ya dunia katika uzalishaji wa madini hayo ni kuongeza manufaa kwa wananchi wake kwa kuongeza ajira na mchango wa sekta kwenye uchumi.

Pia, Mhe. Mavunde alieleza kuwa kutokana na umuhimu huo, Tanzania ipo mbioni kuanza utekelezaji wa programu ya utafiti wa kina wa madini yenye lengo la kuongeza eneo lililofanyiwa utafiti wa kina kutoka asilimia 16 hadi kufikia asilimi 50 ifikapo mwaka 2030. 

“Hatua hii ina lengo la kuhakikisha kama Nchi tunapata uwekezaji stahiki kwenye uvunaji wa rasilimali zetu na kuchochea uanzishwaji wa viwanda vya uongezaji thamani ndani ya nchi” aliongeza Mhe. Mavunde.

Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde alikitaja Kituo cha Utafiti wa Jiosayansi (African Minerals and Geosciences Centre – AMGC) kilichopo Kunduchi Jijini Dar es Salaam kuwa ni nyenzo muhimu ambayo Nchi za Afrika zinayo nafasi ya kukitumia ili kuimarisha tafiti na uongezaji thamani wa madini mbalimbali, kwani Kituo hicho ni Mali ya Nchi zote za Afrika.

Mkutano huo uliandaliwa na African Strategic Mineral Group (ASMG), ambapo kwa sasa Serikali ya Shirikisho ya Jamhuri ya Nigeria ndiye Mwenyekiti.