Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu imeitaka Serikali kuongeza usimamizi kwa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya miundombinu jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na viwango vilivyokubaliwa kwenye mikataba.

Kamati hiyo imeeleza kuridhishwa kwake na kasi ya ujenzi wa daraja la Jangwani na kutaka kasi zaidi kwenye miradi ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT)4 .

 Mwenyekiti wa Kamati hiyo Selemani Moshi Kakoso ameitaka Serikali kuondoa changamoto zinazokwamisha kazi na kuwawajibisha wakandarasi wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa mikataba.

“Kamati imeridhishwa na namna mradi wa daraja la Jangwani unaogharimu takribani Shilingi bilioni 97 unavyosimamiwa, na kusisitiza umuhimu wa kuimarisha usimamizi ili ukamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa” amesema Mhe. Kakoso.

Aidha, ameitaka Serikali kuhakikisha wakandarasi wanaongeza nguvu kazi, wataalamu, mitambo na muda wa kazi ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo ya Miundombinu imeishauri Serikali kuweka utaratibu wa kutoza ada kwa watumiaji wa baadhi ya miundombinu mikubwa, ikiwemo daraja la Tanzanite, ili kupata vyanzo vipya vya mapato vitakavyosaidia kugharamia ujenzi wa madaraja na barabara nyingine nchini.

“Serikali inapaswa kuongeza ushirikiano na sekta binafsi katika ujenzi wa barabara na madaraja makubwa kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), akieleza kuwa mfumo huo unaweza kusaidia kuharakisha upatikanaji wa miundombinu ya kisasa na kupunguza mzigo wa kifedha kwa Serikali,”ameeleza Kakoso.

Amesisitiza umuhimu wa wakandarasi wanaotekeleza miradi mikubwa kuacha alama za maendeleo kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya miradi kupitia uwajibikaji kwa jamii (CSR), akipendekeza ujenzi wa vituo vya afya, shule au huduma nyingine muhimu kama sehemu ya mchango wa miradi hiyo kwa jamii iliyotoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wake.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi, Godfrey Kasekenya amesema Serikali imepokea maelekezo na ushauri uliotolewa na Kamati na itaendelea kuyafanyia kazi, akieleza kuwa ziara hizo ni muhimu katika kuhakikisha fedha zinazotengwa kwa miradi ya maendeleo zinatoa thamani halisi kwa wananchi na miundombinu inayojengwa inakidhi viwango vilivyokusudiwa.

Ameeleza kuwa Serikali pia ina mpango wa kujenga barabara mpya itakayotoka eneo la Bandari ya Dar es Salaam kupitia Kigamboni- Chanika -Kisarawe hadi Kiluvya hatua inayolenga kupunguza msongamano wa magari yanayotoka bandarini kuelekea mikoani.

 “Mradi huo ni sehemu ya mpango mpana wa kujenga barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dar es Salaam (Outer Ring Road), huku Serikali ikitarajia kuanza kuona hatua za utekelezaji mapema mwaka 2027,”amesema Kasekenya.

Kuhusu mradi wa daraja la Jangwani, Naibu Waziri Kasekenya amesema usanifu umezingatia changamoto za mafuriko katika eneo hilo, ambapo urefu na kimo cha daraja vimeboreshwa ili kuruhusu maji kupita kwa urahisi na kupunguza hatari ya mafuriko maeneo ya Jangwani na Kariakoo.