Na OWM-TAMISEMI, Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) imeanza kupitia viashiria vya kupima utendaji wa Halmashauri katika usimamizi wa taka ngumu na usafi wa mazingira, ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ongezeko la taka, kulinda afya ya wananchi na kuweka mazingira ya Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Akifungua kikao kazi cha siku mbili leo Septemba 22, 2026, jijini Dodoma, Mratibu wa Huduma za Afya na Usafi wa Mazingira kutoka OWM-TAMISEMI, Bwana Selemani Yondu, amesema mapitio hayo yanalenga kuweka viashiria vinavyoeleweka na kupimika ili kutathmini kwa usahihi utendaji wa kila Halmashauri.
Kwa mujibu wa Taarifa ya Mwaka ya Utendaji wa Usimamizi wa Takangumu 2025/2026, Tanzania Bara inazalisha wastani wa tani 666,604 za taka ngumu kwa mwezi, lakini tani 368,665 pekee, sawa na asilimia 55.3, ndizo zinazokusanywa, huku tani 297,939 zikibaki bila kukusanywa. “Ingawa asilimia 97.6 ya taka zinazokusanywa hufikishwa katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya utupaji, bado karibu nusu ya taka zinazozalishwa nchini hazikusanywi,” amesema Yondu.
Taarifa hiyo inaonesha kuwa Halmashauri za Manispaa zinaongoza kwa kukusanya asilimia 72 ya taka, zikifuatiwa na Majiji kwa asilimia 70.1, Miji asilimia 50.9 na Wilaya asilimia 45.5. Bwana Yondu alisema uwekezaji zaidi unahitajika katika Halmashauri za Wilaya na Miji zinazokabiliwa na upungufu wa magari, vifaa, fedha na maeneo rasmi ya utupaji. “Halmashauri za Wilaya zinaunda asilimia 73 ya Halmashauri zote nchini; hivyo, mafanikio ya kitaifa hayawezi kupatikana bila kuimarisha uwezo wake,” amesisitiza.
Kwa upande wa miundombinu, asilimia 15 pekee ya Halmashauri kati ya 184 dio zenye madampo ya yanakokidhi mahitaji, huku asilimia 12 zikiwa hazina maeneo rasmi ya kutupa taka. Aidha, asilimia 90 ya Halmashauri zina sheria ndogo za usimamizi wa taka na asilimia 86 zimeweka ada na tozo, lakini asilimia 53 pekee ndizo zinazotenga mapato hayo kwa ajili ya kuendeleza huduma.
Kwa upande wake Bi. Maua Hayeshi Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti wa Takangumu Manispaa ya Kigamboni, mkoani Dar es Salaam alisema katika kudhibiti takangumu, maji taka na usafi wa mazingira, unahitajika ushirikiano wa karibu baina ya kitengo chake na Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii pamoja na kuwepo kwa mfumo wa usimamizi wa taka kuanzia ngazi ya mtaa hadi Taifa
Kikao hicho cha siku mbili kimewahusisha wataalamu kutoka OWM-TAMISEMI, Maafisa Afya wa Mikoa na Halmashauri pamoja na Wakuu wa Vitengo vya Udhibiti wa Taka, ambao wanapitia viashiria vya ukusanyaji wa taka, miundombinu, vifaa, fedha, utekelezaji wa sheria ndogo na ushiriki wa sekta binafsi.

