Na Mwandishi wetu, NAMTUMBO

MGOGORO wa ardhi uliodumu kwa takribani mwaka mmoja na kuhusisha eneo la hekari 51 katika Kijiji cha Songambele, Kata ya Mchomoro, Wilaya ya Namtumbo, umefikia mwisho baada ya pande mbili zilizokuwa zikigombania ardhi hiyo kufikia makubaliano ya amani kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.

Mgogoro huo ulihusisha Serikali ya Kijiji cha Songambele na mwananchi Mustapha Njikwile, ambaye alikuwa akidai haki ya kutumia eneo hilo ambalo alikuwa amelima kwa muda mrefu kabla ya kuondoka katika kijiji hicho.

Akizungumza kuhusu utatuzi wa mgogoro huo, Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Songambele, Ally Yassin Mikila, amesema chanzo cha mgogoro huo ni kutokuelewana kuhusu mashamba yaliyokuwa yakitumiwa na Njikwile kabla ya kuondoka katika kijiji hicho.

Amesema baada ya Njikwile kuondoka, Serikali ya Kijiji cha Songambele ilichukua maeneo hayo na kuyaingiza katika Mpango wa Matumizi ya Ardhi wa Kijiji, hatua iliyosababisha kutokea kwa mgogoro huo.

“Tunashukuru Kampeni hii ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia kwa kutusaidia kutatua mgogoro huu kwa njia ya amani na upendo,” amesema Mikila.

Ameeleza kuwa baada ya Njikwile kuwasilisha malalamiko yake kupitia Kampeni hiyo, wataalamu wa sheria walifika katika eneo la mgogoro na kusikiliza maelezo kutoka pande zote mbili, hatua iliyowezesha suala hilo kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Afisa Sheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Christopher Kabado Kabado, amesema baada ya kufanyika kwa uhakiki na majadiliano baina ya pande hizo, Serikali ya Kijiji imekubali kumpatia Njikwile jumla ya hekari 51 kwa ajili ya shughuli za kilimo.

Amesema mgogoro huo umetatuliwa kwa kutumia Njia Mbadala ya Utatuzi wa Migogoro (ADR), ambapo pande zote mbili zimefikia makubaliano ya amani na hivyo kuhitimisha mgogoro huo uliodumu kwa takribani mwaka mmoja.

Kabado amezipongeza Serikali ya Kijiji cha Songambele na Njikwile kwa kushirikiana katika kutafuta suluhisho la mgogoro huo na kufikia makubaliano ya amani.

Aidha, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha wananchi kupata huduma za msaada wa kisheria kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.